NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuhakikisha wanaandika habari kwa kuwianisha pande zote na kusimamia maadili ya taaluma, akisisitiza kuwa kutofanya hivyo ni kukosa uadilifu na kwenda kinyume na misingi ya uandishi wa habari.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 23,2025 Msigwa amesema kuwa katika siku za karibuni kumekuwapo na tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kutoka nje ya nchi kuchapisha tuhuma zinazoihusu Serikali bila kuipa nafasi ya kujibu, jambo ambalo ni kinyume na maadili na linaweza kupotosha umma.
Amesema si haki kwa chombo cha habari kuchapisha taarifa zilizojaa tuhuma dhidi ya serikali ya Tanzania bila kuipatia nafasi za kujibu na kuzitolea uafafanunuzi.
“Si haki kuchapisha tuhuma bila kumpa mlengwa nafasi ya kujibu, si sahihi chombo cha habari kuchapisha taarifa za upande mmoja Kisha kudai kuwa maofisa wa Serikali hawakupatikana, Serikali ipo wazi, inawajibika kwa wananchi, na iko tayari kutoa taarifa sahihi kwa wakati wowote. Kujenga taifa linaloamini katika ukweli kunahitaji waandishi wenye uadilifu,” amesema Msigwa.
Amefafanua kuwa waandishi wa habari wana jukumu kubwa kuhakikisha kuwa taarifa wanazoandika zinatokana na ukweli, uhakika na vyanzo vinavyoaminika, si hisia au mitazamo binafsi.
Aidha, Msigwa ameelezea kwa kina kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo miradi mikubwa ya miundombinu, nishati, elimu, afya na sekta ya maji.
Akizungumzia kuhusu matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na tarehe zilizofuatia, Msigwa
amesema Serikali imesikitishwa na matukio hayo yaliyosababisha vifo, mauaji, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema Serikali inatoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao, wanaombea majeruhi uponyaji na kwamba wanatoa pole kwa waliopoteza mali zao.
“Serikali inatoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu, walioumia na wote walioathirika na matukio ya Oktoba 29. Haya ni matukio ya kusikitisha hivyo tusiruhusu raia kutoka nje ya nchi kuja kutuvuruga na kuharibu Amani yetu,” amesema
Amesisitiza kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda Tume Huru ya kuchunguza matukio hayo na imepewa muda wa miezi mitatu kuhakikisha inakuja na ripoti itakayojibu maswali yanayouliza na wananchi wakiwemo vijana.
“Tayari Rais ameshaunda tume huru ambayo imepewa miezi mitatu inakwenda kuchunguza matukio yote yaliyotokea Oktoba 29,2025 , tuipatie muda itakuja na majibu ya maswali yote,” amesema Msigwa
Hata hivyo Msigwa amesisitiza kuwa kazi za waandishi wa habari wa ndani ya nchi ndiyo sahihi, tofauti na kazi za waandishi wa vyombo vya habari kutoka nje ya nchi ambao baadhi yao wamekuwa wakichapisha taarifa zilizojaa tuhuma dhidi ya Serikali ya Tanzania bila ya kuipa nafasi ya kuzitolea ufafanuzi.
“Ndugu zangu, nimezungumza kwa utu, ili kuwaambia mnachokifanya ni sahihi na mimi kazi yenu ninaiona, mnapotukosoa mnatukosoa, mnapoona pamekwenda sawasawa mnaandika. Na mimi nataka niwaambie waandishi wa habari msidhani hili jambo linafanywa kwa bahati mbaya ni kwa makusudi,” amesema Msigwa.

