NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM
WANAWAKE nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika siasa, uongozi na upigaji kura kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Wito huo umetolewa na Muungano wa Asasi za wanawake na watetezi wa usawa wa kijinsia ambao wameeleza kuwa ushiriki wa wanawake ni nguzo muhimu ya kukuza demokrasia jumuishi na maendeleo endelevu ya taifa.


Akisoma tamko hilo jijini Dar es Salaam, Rose Mwalimu kutoka Tanzania Media Women Association (TAMWA) amesema huu ni wakati wa taifa kuthibitisha kuwa uongozi bora haupimwi kwa jinsia, bali kwa uwezo, maadili na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
“Tunawahimiza wanawake wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29. Ni fursa ya kuchagua viongozi watakaosimamia ajenda za maendeleo zinazogusa maisha ya wanawake na watoto,” amesema Mwalimu

Kwa upande wake, Lucy Kilasi kutoka Women Welfare Tanzania (WWT) amesema mwaka huu Tanzania imepiga hatua kubwa katika usawa wa kijinsia kisiasa, akibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anawania tena urais kupitia CCM, huku wanawake wengine wawili ,Saumu Rashid (UDP) na Mwajuma Mirambo (UMD) wakijitokeza kuwania nafasi hiyo.
Amesema hatua hiyo inaashiria kuwa jamii inaanza kuamini uwezo wa mwanamke kushika nafasi za juu za uongozi.

“Hii ni hatua muhimu katika historia ya siasa ya Tanzania. Inaonesha kuwa jamii inaanza kuamini uwezo wa mwanamke kushika nafasi za juu za uongozi,” amesema Lucy Kilasi.
Aidha, amekemea vitendo vya kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi dhidi ya wanawake wanasiasa, akisema vitendo hivyo vinadhoofisha motisha na ushiriki wao katika siasa.
“Mwanamke kiongozi asihukumiwe kwa jinsia yake, bali kwa uwezo na dira yake ya maendeleo. Uongozi wa mwanamke si tishio, ni fursa ya demokrasia jumuishi,” amesisitiza.
Muungano huo pia umeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama, huru na yasiyo na vitisho vya kijinsia, huku vyombo vya habari vikitakiwa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake na kuratibu mijadala inayojenga uelewa wa umma kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

