NA MWANDISHI WETU,NAIROBI,KENYA

WACHEZAJI wa Timu ya Tiafa ya Gofu ya Wanawake Neema Olomi, Vicky Elias, Khadija Selemani, Shufaa Twalib wakiongozwa na Meneja wa timu hiyo Yasmin Chali wapo nchini Kenya kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika Mashindano ya Gofu kwa Wananawke Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (EACAACT).
Wachezaji hao wameondoka nchini Jumapili ya Oktoba 19, 2025 na wataiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo yanayotimua vumbi viwanja vya Great Rift Valley Lodge & Golf Resort vilivyopo Naivasha, Kenya.

Katika mashindano hayo yatakayoanza Oktoba 22 na kumalizika Oktoba 24, 2025, yameshirikisha pia wachezaji wa gofu wanawake kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda, Madagascar na Reunion.
Meneja wa timu hiyo Chali amesema kuwa wachezaji walioenda mwaka huu baadhi yao ni mara ya kwanza wanaingia katika timu na hiyo imetokana na wachezaji hao kufanya vizuri katika michuoani mbalimbali nchini.
Amesema kwa ujumla wachezaji wao wamepata siku tatu za kufanya mazoezi hapo Kenya kabla ya kuanza kwa mashindano lengo ni kuzoea kiwanja na kwamba wanaimani kuwa watafanya vizuri katika michuano hiyo.
“Hata hvyo tunaishukuru Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na wadau mbalimbali kwa kufanikisha wachezaji hawa kushiriki michuano hii ambayo itawaongezea fursa wachezaji wetu kubadilishana uzoefu wao na kubadilishana Mawazo,” amesema
Mwenyekiti Umoja wa Wanawake Wachezaji wa Gofu, Rosemary Mkok amesema anawakaribisha washiriki wote katika michuano hiyo yenye hadhi kubwa ambayo huwakutanisha wachezaji bora kutoka katika nchi mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema wanatarajia kuwa michuano hiyo italeta ushindani wa hali ya juu, kuongeza urafiki na kubadilishanaji wa tamaduni na kwamba timu yao ya maandalizi imejipanga kuhakikisha tukio hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa, likiwa na miundombinu bora, ukarimu wa hali ya juu na mazingira yanayoakisi hali halisi ya mchezo wa gofu.

