NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimepata ithibati na kuthibitishwa rasmi na Wakala wa Usalama wa Anga wa Ulaya (European Aviation Safety Agency -EASA) kuwa Kituo cha Mafunzo na Mitihani ya leseni za kimataifa kwa wahandisi matengenezo ya ndege.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi wakati akizindua rasmi kituo hicho ambapo amesema NIT kitakuwa kituo cha mafunzo ya Uhandisi Matengenezo ya Ndege (EASA Part -147 Maintenance Training Organization).
Amesema hatua hiyo iliyofikiwa na NIT inakifanya chuo hicho kutambulika kimataifa na kwamba hayo ni mafanikio ya kipekee na ya aina yake ambayo yatawezesha kupatikana kwa wataalamu wenye ubora na vigezo stahiki za ushindani katika soko la kikanda na kimataifa.

“Serikali katika chuo hiki imewekeza kiasi kikubwa sana, tumetembelea majengo na kuona vifaa vya kisasa, huu ndio mwanzo mzuri wa kuzalisha wataalamu wenye ubora ambao tumekuwa tukiwakosa kwa muda mrefu, kama mnavyofahamu nchi yetu imekuwa na uhaba wa marubani hali inayofanya kutafuta wataalamu hao kutoka nchi za nje na kuwalipa fedha nyingi.

“Pia tunauhaba wa wahandisi wa matengenezo ya ndege ambao unakuta tunawafundisha kwenye vyuo vya nje Ethiopia, Marekani na Canada hivyo tunapoteza fedha nyingi za kigeni, hata hivyo kwa hatua hii iliyofikiwa na NIT, wataalamu hawa watazalishwa hapa hapa nchini na tutaweza kuokoa fedha za kigeni ambazo tulikuwa tunazitumia kwa wingi nje ya nchi,” amesema Msangi

Hata hivyo Msangi amewataka wazazi kuwahamasisha watoto wao kusoma masomo ya sayansi ili kupata fursa ya kusoma urubani, uhandisi matengenezo ya ndege katika chuo cha NIT na hatimaye Taifa kupata wataalamu wa kutosha.

“Chuo cha NIT ni kikubwa na kinahitaji wanafunzi wa kutosha hivyo watanzania tutumie fursa ya kuwaleta watoto kwa wingi kuja kusoma ili nchi ipate wataalamu wa kutosha,” amesema

Naye Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Mgaya amesema chuo hicho kimefikia hatua hiyo kutokana na uwekezaji mkubwa wa fedha uliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mafunzo ya usafiri wa anga ni gharama na watanzania miaka mingi wamekuwa wakitamani kupata mafunzo ya urubani, uhandisi matengenezo ya ndege hapa nchini, lakini wamekuwa wakishindwa kwa sababu yamekuwa yakipatikana nje ya nchi.

“NIT tulipoanza kutoa mafunzo watanzania wengi wamekuja ili kuweza kusoma lakini kama mnavyofahamu usafiri wa anga unasimamia kimataifa, kutambulika kwa chuo chetu na EASA hii ni hatua kubwa nchini kwani atakayemaliza mafunzo hapa ataweza kuajiliwa katika mshirika mbalimbali ya kimataifa bila kufanya mitihani mengine,” amesema Dk. Mgaya na kuongeza

“Mafunzo hayo yatakayotolewa NIT sasa yanatambulika kimafaita hivyo lazima tuwe na wakufunzi pia wanaotambulika kimataifa, kwa bahati nzuri leo wakufunzi wetu nane wamepata vyeti vya kutambulika na EASA kuwa wanafaha kutoa mafunzo hayo ya uhandisi matengenezo ya ndege,” amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Aerolink, Mhandisi wa Ndege Edith Kisamo amesema Tanzania inajivunia kuwa na kituo cha kwanza cha mafunzo na mitihani cha EASA kilichopo NIT ambacho kitatoa fursa kwa vijana wa kitanzania na nchi jirani kusoma masuala ya anga kwa gharama nafuu.
“Hayo si mafanikio ya taasisi peke bali ni ushahidi wa kile kinachowezekana pale tunapowekeza katika uwezo wa watanzania, wajibu wa Aerolink umekuwa ni kujenga daraja, kuunganisha utaalamu wa anga,” amesema Kisamo
Aidha amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imewekeza katika miundombinu ya kisasa katika chuo hicho na Aerolink imehakikisha kuwa uwekezaji huo haushii kwenye majengo bali unawekezwa katika ubongo wa kijana wa kitanzania.

