NA MWANDISHI WETU,UYOLE,MBEYA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendesha mpango wa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea mbadala kulingana na aina ya zao na mahitaji ya udongo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa kilimo wa 2025/2026.

Elimu hiyo imetolewa na wataalam wa TFRA wakiongozwa na Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi, Chrysantus Funda, ambaye amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija kwa wakulima.

Kikao hicho maalum kimefanyika Oktoba 03, 2025 katika Bonde la Uyole, mkoani Mbeya, na kimewakutanisha wakulima wa maeneo hayo kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya usimamizi wa mbolea.

Umuhimu wa mpango huu, kwa mujibu wa TFRA, ni kuwaelimisha wakulima kuhusu aina ya virutubisho vinavyohitajika katika udongo na mazao yao, ili kuepuka hasara na kuongeza mavuno bora. Pia unalenga kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi ya matumizi ya pembejeo.
Funda alibainisha kuwa kila udongo una mahitaji tofauti ya virutubisho, hivyo wakulima wanapaswa kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea. Alisema uelewa huo utasaidia kuongeza mavuno na ubora wa mazao.

Aidha, aliwataka wakulima kuachana na tabia ya kutumia mbolea ileile kila msimu bila kuzingatia mabadiliko ya udongo, zao na hali ya hewa, akisema mtindo huo unasababisha kupungua kwa tija.
Kwa upande mwingine, TFRA imewahimiza wakulima kujisajili kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku unaosimamiwa na serikali, huku ikiahidi kusimamia kwa karibu mawakala wote ili kuhakikisha bei halali zinabandikwa kwenye maduka yao.
Aidha, Mamlaka hiyo imesisitiza itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti na kilimo kama TARI na THPA ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa endelevu, yenye tija na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

