NA MWANDISHI WETU, LINDI
SERIKALI imeeleza kutambua na kuthamini mchango ya wadau wanaochagiza maendeleo ya elimu katika shule za sekondari hususani katika kukuza sayansi na ubunifu kwa vijana wanaoonesha vipaji vya sayansi na ubunifu.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva wakati wa maonesho ya sayansi na gunduzi za kiteknolojia yaliyoandaliwa na kuratibiwa Mkoani Lindi na Shirika la Wanasayansi (YST) kwa udhamini wa Kampuni ya Shell Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Lindi mjini, Mwanziva ameipongeza YST kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhamasisha wanafunzi kupenda sayansi na kuwa wabunifu wa kutengeneza miradi mbalimbali ya kisayansi ya kuleta tija kwa jamii hususani katika karne hii iliyojaa ushindani wa bunifu za kiteknolojia.

Amesema wanaipongeza YST na Kampuni ya Shell kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza na kuendeleza sekta ya elimu Mkoani Lindi hasa kwa kuibua vipaji vya wanafunzi katika sayansi na teknolojia kwenye kada ya sayansi jamii, fizikia, baiolojia, na kemia hatua itakayosaidia kutupatia wataalamu wa kada mbalimbali katika nchi.
“Maonesho haya vipaji vya wanasayansi, yakawe chachu ya kuzidi kuwainua wanafunzi wetu katika kufanya sayansi ya vitendo na yenye kuiletea tija Taifa letu kwenye maeneo mbalimbali ya maendeleo,” ameeleza Mwanziva na kuongeza


“Yote yaliyowasilishwa Serikali imeyachukua na itayafanyia kazi ili kuhakikisha msingi huu wa elimu na ujuzi unaendelezwa, pia Serikali itaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo YST katika kutafuta na kuwapatia wanafunzi fursa za kujiendeleza kielimu hususani katika sayansi ili wawe na tija katika uchumi,” ameeleza
Kwa upande wake Mshauri wa Masuala ya Kijamii Kampuni ya Shell Tanzania, Msomisi Mbena amesema kuwa katika karne hii ya sasa sayansi ni hitaji kubwa katika nchi ili kuweza kujenga uchumi ulio imara, na ndiyo maana wameamua kuwekeza katika jitihada hizi za kuzalisha wanasayansi chipukizi ili waweze kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa YST imekuwa ni Taasisi ya mfano inayotoa mchango chanya katika kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kubuni miradi inayoleta suluhisho dhidi ya changamoto mbalimbali kwenye Afya, kilimo, mazingira, maji, mifugo, elimu na maeneo mengine.
Akimwakilisha Mwanzilishi mwenza wa YST, Meneja mradi Nabil Karatela amesema kuwa YST inatambua umuhimu wa mchango wa sayansi katika kuchochea maendeleo ya vijana kiuchumi, pia jitihada hizi zinalenga kuwawezesha vijana kuwa washindani kwenye teknolojia.
Amesema kuwa mashindano haya yanalenga kuibua vipaji vya wanafunzi katika kuweza kubuni masuluhisho yanayoweza kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii wanayoishi.
Katika mashindano haya jumla ya shule tatu bora kutoka Mkoa wa Lindi ambazo ni shule ya Sekondari Kibutuka, Kiranjeranje na Nachingwea ziliibuka washindi wa mashindano, na kuchaguliwa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya jumla yanayotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Nachingwea Igalu Mussa amesema mashindano haya yanawapa changamoto nzuri katika masomo yao kwa kuwawezesha kujua namna ya kutumia sayansi kubuni vitu katika uhalisia wake na pia kubuni miradi inayoleta utatuzi katika maeneo mbalimbali ya jamii yao ikiwemo kwenye uvamizi wa mifugo katika mashamba ya wakulima.

