NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kuendeleza jitihada za kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea na kuwafikia wakulima moja kwa moja, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanikiwa kuwahudumia zaidi ya wakulima elfu moja katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA )yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28 na kufikia tamati Julai 13 Julai, 2025.
Wakulima hao waliotoka ndani na nje ya Tanzania walitembelea banda la TFRA na kunufaika na elimu, huduma na fursa mbalimbali zilizotolewa na Mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na usajili katika mfumo wa kidijitali wa pembejeo za ruzuku, elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, pamoja na huduma za ushauri kuhusu aina bora za mbolea kulingana na mahitaji ya mazao.
USAJILI WA WAKULIMA NA LESENI KWA WADAU
Miongoni mwa mafanikio ya TFRA katika maonesho hayo ni kusajili wakulima 127 kwenye mfumo wa Kidijitali wa pembejeo za ruzuku, hatua inayowawezesha kunufaika moja kwa moja na mbolea kwa bei nafuu inayotolewa na Serikali. Vilevile, wadau 85 wa biashara ya mbolea walipata elimu ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Mbolea (FIS) na kuhuisha leseni zao kwa haraka na kwa urahisi.
DIRA YA 2030:TANZANIA KUWA KITOVU CHA MBOLEA AFRIKA
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, alibainisha dhamira ya Serikali kupitia TFRA ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Alisema kufanikisha dira hiyo kutategemea kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa viwanda vya ndani, usafirishaji wa pembejeo nje ya nchi na upatikanaji wa mbolea kwa wakati kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Laurent, matumizi ya mbolea nchini yamepanda kwa kasi kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi kufikia takriban tani milioni moja kwa msimu wa 2024/2025, jambo linaloonesha mafanikio ya wazi katika utekelezaji wa sera za kilimo.
UBUNIFU,USHIRIKIANO NGUZO YA MAFANIKIO
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA, Dk. Peter Shimo, amepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya TFRA na taasisi nyingine chini ya Wizara ya Kilimo katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Dk. Shimo alisisitiza kuwa elimu hiyo ni msingi imara wa kuongeza uzalishaji na kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
FURSA KATIKA UHAMASISHAJI MBOLEA
Naye, Meneja Uhamasishaji, Uzalishaji wa ndani na Mazingira, Getrude Ng’weshemi, alieleza kuwa kuna fursa kubwa ya kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi. Uzalishaji wa ndani utasaidia kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje, hali itakayochangia kupunguza gharama za mbolea na kuhakikisha upatikanaji wake kwa wakati kwa wakulima.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) imejipanga vizuri kuhakikisha mazingira bora na rafiki kwa uwekezaji. Tunawahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hii, kwani Tanzania ina sera thabiti, miundombinu inayoboreshwa kila siku, na soko la uhakika la wakulima wanaohitaji mbolea kwa wingi.
ELIMU KWA WANANCHI MBINU SAHIHI ZA KILIMO
Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Aziz Mtambo, alisema wananchi wengi walihamasika kutembelea banda la TFRA kutokana na ubora wa huduma walizozipata, ikiwemo elimu ya kutosha kuhusu aina za mbolea za kupandia na kukuzia, pamoja na umuhimu wa kutumia mbolea zilizosajiliwa rasmi.
Mtambo alieleza kuwa wakulima pia walifundishwa kuhusu usalama wa uhifadhi wa mbolea, umuhimu wa kusoma maelekezo ya matumizi, na namna ya kutambua mbolea bora, kwa lengo la kuhakikisha kilimo endelevu na chenye tija.
USHUHUDA WA WAKULIMA
Wakulima kutoka maeneo mbalimbali nao walipata fursa ya kueleza maoni yao juu ya huduma walizopata kutoka TFRA, Mkulima George Masanga kutoka Ruvuma aliieleza kuwa alipata fursa ya kusajiliwa kwenye mfumo wa ruzuku baada ya kukosa nafasi hiyo huko alikotoka kutokana na umbali. “Huduma hii itanisaidia sana msimu ujao. Nimejifunza pia matumizi sahihi ya mbolea na ninaamini nitazalisha zaidi,” alisema.
Hassan Mambo kutoka Dar es Salaam alisisitiza umuhimu wa wakulima kujitokeza kwenye maonesho kama haya ili kupata elimu muhimu. “Watu wengi hawajui kuwa mbolea zinapimwa na kuthibitishwa ubora wake kabla ya kuingia sokoni. TFRA inatoa elimu hii kwa uwazi kabisa,” aliongeza.
Kwa upande wake, Daudi Sanga kutoka Njombe alitoa wito kwa Serikali kuendelea kusogeza huduma za pembejeo karibu zaidi na wakulima hasa vijijini, ili waweze kulima kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Maonesho ya SABASABA yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na kuwapa fursa ya kupata maarifa ya kisasa, hasa katika sekta ya kilimo. Kupitia TFRA, wakulima si tu walipata elimu bali pia walifunguliwa milango ya fursa ambazo zitawawezesha kuongeza uzalishaji, kipato na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Kwa mafanikio haya ya mwaka 2025, TFRA imeonesha dhamira ya kweli ya kuendeleza mapinduzi ya kilimo kupitia mbolea bora, elimu sahihi, na mifumo ya kidijitali inayowafikia wakulima moja kwa moja vijijini na mijini.