*NI KIWANDA KIKUBWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI
*NI UZINDUZI WA KIHISTORIA
NA MATILDA KASANGA
KUFUATIA kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha itracom ulioanza mnamo mwezi Julai, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Samia Suluhu Hassan anakwenda kuzindua kiwanda hicho.
Uzinduzi wa kiwanda hicho unakwenda kuandika historia mpya inayopelekea nchi ya Tanzania kuwa kitovu cha mbolea Afrika Mashariki na Kati na kupunguza utegemezi wa mbolea zinazoingizwa kutoka nchi za nje.
Akitoa taarifa ya uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari hivi karibuni, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameeleza kuwa kiwanda hicho kilichopo Nala jijini Dodoma kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka huku akibainisha kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea za mchanganyiko za kikaboni na madini (organo-mineral fertilisers) kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima.
Bashe anasema, kwa kipindi kirefu nchi imekuwa ikiagiza takribani tani milioni 1.2 kutoka nje ya nchi lakini uwepo wa kiwanda cha Itracom ambacho ni kikubwa Africa Mashariki kikiwa na uwekezaji wa jumla ya dola milioni 180 ambapo tayari kimeanza uzalishaji na baadhi ya wakulima wameshanufaika na mbolea inayozalishwa na kiwanda hiki.
Kupitia mazingira bora ya uwekezaji, sekta ya mbolea nchini imekuwa na maendeleo makubwa kwa kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa zaidi cha mbolea nchini — ITRACOM Fertiliser Limited (IFL) kilichopo Dodoma.
ITRACOM ni kampuni Waziri wa Kilimo, Hussein Mohamed Bashe anasema serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.
Kwa kuwa na dhamira hiyo ya kisiasa, wawekezaji wamekuwa wakinufaika na vivutio mbalimbali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ikiwemo upatikanaji wa ardhi, msamaha wa kodi kwa mitaji ya miradi ya viwanda vya mbolea, punguzo la kodi kwa mitaji ya miradi ya uchimbaji wa malighafi, pamoja na posho za mitaji na uondolewaji wa kodi kwenye thamani iliyopungua.
Kupitia juhudi hizo, uwekezaji mpya kama ule wa ITRACOM wenye thamani ya dola milioni 180 umeweza kuanzishwa, ukiwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,000,000 kwa mwaka, na matarajio ni kufikia tani 1.2 milioni mwaka ujao.
Mafanikio haya si bure, Serikali imeweka juhudi kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira na sera Rafiki zinazowavutia wawekezaji kuwekeza nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa kilimo katika ukuaji wa uchumi, usalama wa chakula na lishe, pamoja na kupunguza umaskini, na kwa kuzingatia kwamba mafanikio ya kilimo yanategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mbolea ikiwa ni miongoni mwa mahitaji hayo, serikali imeendelea kuvutia wawekezaji wa kigeni kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha mbolea.
Lengo kuu la serikali ni kuifanya Tanzania kuwa Kitovu cha mbolea kwa kufungua soko la mbolea kwa nchi jirani na kuongeza upatikanaji wa mbolea kwa wakulima ili waweze kuongeza tija ya kilimo na kuboresha maisha yao.Maono hayo yamepelekea idadi ya viwanda vinavyozalisha mbolea na virutubisho vya mbolea nchini kuongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka minne iliyopita kutoka viwanda 16 mwaka 2020/21 hadi kufikia viwanda 33 mwaka 2023/24.Katika kuhakikisha kwamba azma ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mbolea, baadhi ya viwanda vya mbolea nchini vinaendelea kupanua uwezo wake wa uzalishaji. Kwa mfano, kiwanda cha Minjingu Mines & Fertilizer Limited kimeongeza uwezo wake kutoka tani 100,000 mwaka 2022/23 hadi kufikia tani 250,000 kwa sasa.
Aidha, serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na TIC imesaini mkataba na kampuni ya Indonesia ya Essay Group Limited kwa ajili ya kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea ya Urea kutoka Ammonia kwa kutumia gesi asilia, kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka na kinatarajiwa kuanza kazi rasmi mwaka 2029.
UZINDUZI WA ITRACOM FERTILISER
LIMITED
Jumamosi, Juni 28, wakulima wa Tanzania na wadau wa sekta ya kilimo watashuhudia tukio la kihistoria ambapo Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, wanatarajiwa kuzindua rasmi kiwanda kikubwa cha mbolea cha ITRACOM katika mji mkuu wa utawala, Dodoma.
Waziri Bashe ana imani kuwa uzinduzi rasmi wa kiwanda hicho cha kisasa — ambacho tayari kimeajiri watu 1,805 — utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kuagiza mbolea kutoka nje, kwani uzalishaji wa ndani unatarajiwa kukidhi mahitaji ya taifa ifikapo mwaka 2030, ambapo inakadiriwa kuwa tani milioni 2.1 kwa mwaka zitahitajika.
MCHANGO WA TFRA KWA ITRACOM
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent anasema ili kuhakikisha kiwanda hicho kinatimiza majukumu yake kwa viwango vinavyotarajiwa na wateja wake, TFRA itaendelea kusimamia ubora wa mbolea zinazozalishwa ili ziweze kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, kutimiza mahitaji ya udongo na mazao kulingana na maeneo mbalimbali nchini, na kuhakikisha kuwa uzalishaji wa mazao unalingana na mahitaji ya msimu wa kilimo.
Anasema ni jukumu la Mamlaka yake kuhakikisha ITRACOM inaendelea kuzalisha mbolea ya kutosha kukidhi mahitaji ya wakulima nchini.
“Ni wajibu wetu kuweka mazingira rafiki ya kazi na kuratibu upatikanaji wa malighafi, miundombinu na masoko,” anasema Laurent.
“Ushirikiano wa karibu baina ya TFRA na ITRACOM ni muhimu ili kuhakikisha kunakuwepo na ubora wa bidhaa, uwazi wa bei na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwa wakati unaofaa.”Laurent anaongeza kuwa, ongezeko la mahitaji ya mbolea, eneo la kimkakati la Dodoma katikati mwa nchi na upatikanaji wa malighafi kama jasi na chokaa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Arusha ni miongoni mwa sababu zilizoifanya mwekezaji kutoka nchini Burundikuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda hicho jijini Dodoma.
Anaongeza kuwa, sababu nyingine, ni pamoja na sera rafiki za serikali katika maendeleo ya uchumi wa viwanda, uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji, vivutio vya kikodi, upatikanaji wa ardhi na miundombinu, kujitosheleza kwa chakula na dhamira ya kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha mbolea katika Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza wakati wa mahojiano na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha itracom Nduimana Nazir anashukuru kwa ushirikiano baina ya taasisi zilizoko chini ya Wizara ya kilimo ikiwepo TFRA na TARI na kuwezesha kupatikana kwa aina 14 za mbolea zinazozalishwa na kiwanda kulingana na mahitaji ya udongo na zao.
Anasema kiwanda hicho kinazalisha mbolea tofauti na zile zilizozoeleka na kufanya vizuri shambani huku kiwanda kikiajiri jumla ya wafanyakazi 1805 wa kudumu na 5000 ajira zisizokuwa za kudumu.
Ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kujivunia kiwanda hicho kwa kuhakikisha wanazitumia katika kilimo chao na kuboresha ardhi wanazozilima ili waongeze tija ya uzalishaji.
Wataalamu wa kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki wanasema kuna viwanda vichache vya uzalishaji mbolea, hasa nchini Burundi, Tanzania, na Uganda, huku viwanda vingi vya kuchanganya mbolea vikiwa Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda.
Karibu viwanda vyote vya mbolea vinavyozalisha kwa sasa vinajikita katika mbolea za kemikali, isipokuwa ITRACOM ambayo huzalisha mbolea za mchanganyiko za kikaboni na madini.