NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
NAIBU Mkurugenzi Mtendaji Mipango,Utafiti na Uwekezaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), CPA. Renata Ndege amewataka watanzania kutunza miundombinu ya Shirika hilo na kuacha tabia ya kuchoma laini za umeme na kuiba mafuta ndani ya Transfoma.
Ndege ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha mada katika semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaitarajiwa kufanyika nchini Januari 27 na 28, mwaka huu.
CPA Ndege amesema Shirika lao linaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kulinda miundombinu yao kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi.
Amesema kwa sasa TANESCO katika baadhi ya miundombinu yao wameweka mitambo ya Ulinzi ambayo inateknolojia ya hali ya juu katika ulinzi na endapo mtu akisogea inatambua.
“Tunatamani kuweka mitambo hii katika maeneo mengi lakini kutokana na gharama ya ununuaji wa miundombinu hiyo tunakwenda taratibu katika kuiweka kutokana na gharama hiyo ipo juu.
“Bado tunatumia ulinzi wa kutumia wananchi katika kusaidiana kulinda miundombinu yetu katika maeneo mbalimbali ili kuweza kusaidia miundombinu hiyo kuzidi kuwepo,”amesema.
CPA Ndege amesema kwa sasa TANESCO haina shida ya umeme kutokana na kuwepo kwa miradi mingi ya umeme ambayo inasaidia upatikanaji wa umeme kuwepo katika maeneo mbalimbali.
Amesema umeme unaokatika katika baadhi ya maeneo ni kutokana na ufanywaji wa maboresho na kuongeza uwezo wa yll utoaji wa umeme nchini ambao ni wa uhakika.
“Umeme upo ila tunachofanya ni kuboresha miundombinu yetu na kuongeza uwezo (Capacity)ambayo itasaidia kutoa umeme wa uhakika,”ameeleza
Awali akijibu maswali ya Waandishi wa habari na wahariri,Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati, Innocent Luoga amesema kutokana na uwepo wa miradi mingi nchini hali ya ukatikaji wa umeme unaenda kuisha baada ya miundombinu ya umeme kuimarisha.
“Bado kuna kazi kubwa inaendelea ya kuboresha hali ya umeme kupatikana kwa wakati na mwaka huu baada ya kukamilisha baadhi ya ufungaji wa transformation na hii ni kutokana na miradi kuwa mingi,” amesema