NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MWANAJUMUIYA wa Afrika na Mwanafalsafa kutoka Zimbabwe, Dk. Joshua Maponga, amewataka vijana wa bara la Afrika kuungana na kupambana kuhakikisha Afrika inakuwa moja ili kujenga uchumi imara na kujinasua kutoka kwenye mnyororo wa umaskini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Dk. Maponga amesema kuwa mgawanyiko wa kisiasa, kiuchumi na kifikra miongoni mwa Waafrika umelidhoofisha bara hilo na kulifanya kuendelea kuwa tegemezi licha ya kuwa na rasilimali nyingi.
Amesema kuwa Afrika haiwezi kujijenga kiuchumi ikiwa itaendelea kujiendesha kwa mipaka iliyochorwa na wakoloni, akisisitiza kuwa umoja wa Afrika ndio msingi wa soko kubwa, uzalishaji wa pamoja na matumizi bora ya rasilimali zake.
“Hatutaweza kuondokana na umaskini kama kila nchi itaendelea kujitazama peke yake. Afrika ni nchi moja yenye mikoa tofauti. Tukishikamana, tutakuwa na soko kubwa, nguvu kazi kubwa na sauti moja ya kiuchumi duniani,” amesema Dk. Maponga na kuongeza
“Nataka nijue kutoka kwa vijana wanataka mustakabali gani? Wanafanyaje kuhakikisha mustakabali huo unapatikana? Hii ni nafasi yenu na wakati wenu kubadilisha historia na kuunda Afrika ya kesho. Mtambue kuwa matatizo ya Afrika ni matatizo ya Tanzania. Tunapaswa kuacha kufikiria kuwa tuko katika nchi tofauti, bali tuko katika nchi moja ambayo ni Afrika, lakini tuna mikoa tofauti, na Tanzania ni moja ya mikoa hiyo na mingine ni Zimbabwe, Uganda, Kenya — mikoa yote hii ni sehemu ya Afrika moja.” amesema Dk. Maponga
Aidha amesema kuwa ndoto ya Afrika ya Umoja iliyopandwa na Mwalimu Nyerere, inawahitaji vijana kuitimiza.“Kazi na maisha ya Mwalimu yanaonyesha mwanzo wa ndoto ya Afrika moja. Kazi yake haikuishia Tanzania pekee, bali ilienea kaskazini na kaskazini-magharibi mwa bara. Rafiki yake wa karibu, Kwame Nkrumah, alikuwepo pia katika kuunda ndoto hii ya bara letu la Afrika.” amesema
Hata hivyo Dk. Maponga amebainisha kuwa umoja wa Afrika utasaidia kulinda rasilimali za bara hilo, kuongeza thamani ya bidhaa zake kabla ya kuuzwa nje, pamoja na kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika ambayo kwa sasa bado ni ndogo ukilinganisha na biashara yake na mataifa ya nje.
Mbali na hayo, Dk. Maponga amesisitiza kuwa Tanzania si tu nyumbani kwa viongozi wengi wa kisiasa kutoka ukanda wa kusini mwa dunia huku akisema bila Tanzania, hakuna Afrika Kusini, Zambia, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji, Uganda, wala Kenya.

