NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema maandalizi ya mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika yamekamilika kwa asilimia 70 na kilichobakia kwa sasa ni ufugaji wa taa za barabarani katika baadhi ya maeneo
Aidha Chalamila amewataka wakazi na wafanyabiashara wa jijini la Dar es Salaam kufanya shughuli zao kwa saa 24 ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zitokanazo na Mkutano huo.
Mkutano huo unaotarajiwa kuanza Januari 27 hadi 28 na utafanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha mwalimu Julias Nyerere (JNICC) na kuhudhuriwa na wakuu wa Nchi za Afrika kutoka zaidi ya mataifa 30.
Chalamila ameyamebainisha hayo jijini Dar es salaam katika ziara ya kukagua maandalizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo barabara, kumbi na viwanja vya ndege.
Amesema ni muda muafaka kwa wafanyabiashara kuchangamkia ugeni huo kwa kufanya biashara saa 24 kwani zaidi ya nchi 30 zikitarajiwa kushiriki katika mkutano huo.
“Kufuatia mkutano huo baadhi ya maeneo yameishaanza kufanya biashara saa 24 ..tupo tayari kuwalinda wananchi wote na kuhakikisha wanakuwa salama kwani wageni wetu watahitaji kula chakula, kulala pamoja na kufanya mazoezi”alisema Chalamila
Aidha aliyataka Malori yote yanayopaki kandokando ya barabara ya Nyerere kuondoka mara moja kabla ya Januari 20 na yatafute maengesho mengine.
“Maloli ni kitu kizuri sana kinachotoa ajira, na kuongeza mapato ya nchi lakini yasipowekwa katika utaratibu ni uchafu kama ulivyo uchafu mwingine.”alisema Chalamila nakuongeza kuwa
“Tumekubaliana kwamba kwenye barabarani yaani kwenye uso wa barabara kusiwe na Malori hayo kwa sasa kwani tunadhani hayaleti taswira nzuri hasa tunapoelekea katika kuhakikisha Mji unakuwa safi”alisisitiza
Pia Chalamila alizitaka Mamlaka zote za Halmashauri na Wilaya kuendelea hatua za kuboresha usafi na usalama katika jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.
Kwa upande wa maandalizi Chalamila alisema tayari taa zaidi ya 300 zimeishawasili ambazo zitafungwa katika barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege hadi Posta na maeneo mengine yaliyopangwa.
Aidha alisema baadhi ya barabara zitafungwa huku vyombo vya moto pikipiki na bajaji kutokwenda katika baadhi ya maeneo yatakayotajwa baadaye.