NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
TAKRIBANI watu Milioni 300 katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania wanatarajiwa kufikishiwa nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Januari 5,2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja kuelekea Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika.
Msigwa amesema Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa kama Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na Umoja wa Afrika, wanalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme bora, nafuu, na endelevu kwa Waafrika Milioni 300 kufikia mwaka 2030.
Amesema kupitia mkutano mkubwa wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ambao utafanyika hapa nchini
unalenga kuharakisha ukuaji wa mageuzi katika nishati barani Afrika na kwamba tukio hilo linafanya Tanzania kuwa kitovu cha mjadala wa kimataifa kuhusu nishati ya umeme endelevu.
Msigwa amesema mkutano huo ni matokeo ya juhudi kubwa za kidiplomasia za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Diplomasia ya Rais Kimataifa imeimarisha nafasi yetu kimataifa na kuleta matunda haya tunayoyashuhudia sasa. Na hii ndiyo dhana ya uchumi wa kidiplomasia kwa vitendo. Tunajivunia kuwa sehemu ya mjadala wa huu wa kuwafikishia umeme waafrika milioni 300 kwani hapa ndipo patakaposainiwa andiko hilo na nchi 14 Afrika, huku ukihudhuriwa na Marais zaidi ya 10 wa Afrika,” amesema
“Tanzania ndio wenyeji wa mkutano huu na Kupitia nafasi hii, nchi yetu inaonyesha dhamira yake ya kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya nishati ya umeme barani Afrika, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini na mijini,” amesema Msigwa
Hata hivyo Msigwa amesema umeme ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwamba Kupitia miradi mikubwa wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Tanzania imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa umeme ambao mpaka sasa inazalisha Megawati 1,410 kutoka katika mashine sita na wanatarajia mwaka huu mradi kukamilika.
Amesema kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme, wanawawezesha wananchi na Wajasiriamali kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa, hivyo kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Aidha Msigwa amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024, Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,278, sawa na asilimia 99.7 ya vijiji vyote, Vitongoji 32,827 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,359 sawa na asilimia 51 ikiongeza uwezekano wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Hatua hizi zimeimarisha sekta za elimu, afya, biashara, na usafiri, ambapo taasisi za afya na elimu zaidi ya 12,905 zimeunganishwa na umeme, na kusaidia kuinua viwango vya utoaji huduma kwa wananchi . Zaidi ya hayo, uwekezaji katika vyanzo mbadala vya nishati kama vile umeme jua, jotoardhi, na upepo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa megawati 1,100.
“Juhudi hizi zinalenga kuvutia uwekezaji katika Sekta ya viwanda, ambapo idadi ya viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya nishati kama nguzo na nyaya imeongezeka kutoka 23 mwaka 2020 hadi kufikia viwanda 78 mwaka 2024. Uzalishaji wa ndani wa vifaa hivi si tu unatoa ajira kwa Watanzania bali pia unapunguza gharama za miradi ya usambazaji nishati vijijini na mijini,” amesema
Naye Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga amesema
katika Bara la Afrika takriban watu milioni 685 Kati ya watu zaidi ya Bilioni Moja, bado hawajafikishiwa huduma ya umeme.
Hivyo amesema Mpango wa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ni wa kihistoria utakaosaidia kuharakisha ufikishaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030 kupitia Mpango Mahsusi ujulikanao kama Mission 300.
Amesema mpango huo mahsusi utasainiwa na nchi 14 ambazo ni Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ivory Coast, Burkina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Niger, Nigeria na Zambia.
Hata hivyo Tanzania ambayo inatambuliwa duniani kwa kufanya vizuri katika Sekta ya Nishati itasaini mpango huo mahsusi kwa kuwa ni Nchi Mwenyeji wa Mkutano huo muhimu kwa Sekta ya Nishati.
Hata hivyo amesema Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za maandalizi ya Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaohusu Masuala ya Nishati utakaofanyika katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam, Januari 27 na 28, 2025.
Amesema mkutano huo unaratibiwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Benki ya Dunia (WB) pamoja na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).