NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
KITUO cha Kuendeleza Ubunifu cha Kwanza Hub kinachofanya kazi chini ya Kampuni ya Twigalpha kimewakutanisha vijana wa kizazi cha Generation Z kutoka vyuo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa ubunifu, kujifunza kwa vitendo na hatimaye kupata mtaji wa kuendeleza mawazo yao bunifu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Mkufunzi Idara ya Teknolojia katika kituo hicho, Jenipher Nderumaki alisema lengo la programu hiyo ni kutambua vijana wenye vipaji, wanaojiamini na wanaoweza kufanya ubunifu wa bidhaa pamoja na kujaribu mambo mapya yanayoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Alisema mpango huo ni endelevu kwa kuwa ni moja ya njia ya kupata mawazo mapya ya vijana kuhusu bidhaa zinazotarajiwa kuingia sokoni au ambazo tayari zipo sokoni.
“Kazi yetu ni kutafuta vijana watakaoweza kujadili na kutoa mawazo yao mapya kuhusu bidhaa zilizopo sokoni ili kuziboresha au kuzifanya ziwe na ushindani zaidi,” alisema Nderumaki
Kwa upande wake Mbunifu na Mwanzilishi wa kituo hicho, Mihayo Wilmore alisema programu hiyo inalenga pia kuwasaidia wahitimu wanaoingia katika soko la ajira kujifunza namna ya kubuni suluhisho zitakazobadilisha mifumo ya maisha na biashara.
“Hatuwezi kusema tunajua kila kitu. Tunawaleta hawa Gen Z wafikirie matatizo yaliyopo na jinsi ya kuyatatua ili wabaki kuwa na thamani katika soko, lakini tunataka tufikirie kwa pamoja mimi ambaye nasaidia na wewe kijana mwenye ubunifu kwamba tunafikaje malengo kwa maana kwaba kijana apate kazi na mimi niendelee kuwa na umuhimu katika soko ” alisema.
Naye Meneja Uendeshaji wa Biashara wa kituo hicho, Sia Malewas, alisema kupitia program hiyo vijana 12 walichaguliwa kutoka taasisi tofauti za elimu ya juu, ambapo kati yao watano watakaofanya vizuri zaidi watapatiwa mtaji huo wa kuendeleza miradi yao.
Alifafanua kuwa lengo jingine la programu hiyo ni kuhakikisha kizazi hicho chenye upeo mpana wa fikra kinapata nafasi ya kujifunza, kujenga mahusiano ya kitaaluma na kupata ujuzi wa vitendo hata katika maeneo ambayo hawakusomea darasani.
“Tunawataka vijana wafikirie mambo makubwa na tofauti, kwa sababu tunaamini wana uwezo wa kufikiria zaidi ya yale waliyojifunza darasani,” alisema.
Mmoja wa Majaji wa programu hiyo, Salama Somboka, aliwapongeza washiriki akisema ni vijana wenye uelewa mkubwa, makini, wadadisi na wachapakazi.
Alisisitiza kuwa washindi watano walioibuka bora wana uwezo mkubwa wa kujieleza na anaamini wana safari ndefu ya mafanikio mbele yao.
Aidha, Mmiliki na Mpishi Mkuu wa Mgahawa wa Nico’s Cafe, Nicolaus John, aliwataka vijana kuzingatia lishe bora akisisitiza kuwa vyakula vyenye virutubisho vina mchango mkubwa katika uwezo wa ubongo kufikiri, kubuni na kuleta mawazo yenye tija kwa jamii.
Alisema lishe bora ina uhusiano wa moja kwa moja na ubunifu wa mtu, hivyo aliwashauri vijana kula mlo kamili ili kuongeza umakini na uwezo wa kufikiri kwa kina. Pia aliishukuru KwanzaHub kwa kumshirikisha katika programu hiyo na kumpa nafasi ya kuwaandalia chakula washiriki, akieleza kuwa ni njia nzuri ya kuunga mkono maendeleo ya vijana wabunifu nchini.
Programu hiyo inatarajiwa kuendelea kuwa jukwaa la kuibua vipaji vipya, kukuza ubunifu na kuchochea maendeleo ya suluhisho bunifu yatakayosaidia jamii pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa sokoni.






