NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema kuwa Kilimo cha zao la Mkonge ni cha uhakika hakiathiriwi na mabadiliko ya tabianchi na kwamba kina fursa mbalimbali ikiwemo masoko ya uhakika.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhamasishaji wa bodi hiyo, David Maghali wakati akizungumza na Demokrasia kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba 2024 yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Maghali amesema kwa sasa kuna wakulima zaidi ya 20,000 wanaolima zao la Mkonge nchini na kwamba mahitaji ya zao hilo ni makubwa huku uzalishaji ukiwa bado ni mdogo.
“Niwatoe hofu Watanzania wanaotaka kulima zao hili, kilimo hichi cha mkonge ni cha uhakika kwani hakisumbuliwi na mabadiliko ya tabianchi wala magonjwa lakini mtu ukilima uhakika wa kuuza kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika na bei yake ni nzuri kwani kilo moja ya mkonge unauzwa 3000 hadi 4000 kwa kutegema na daraja,” amesema
Maghali amesema Watanzania waliowengi bado hawajajiunga na kilimo cha mkonge ambacho ni fursa kwa sasa kwani kinaweza kulimwa na wakulima wadogo katika maeneo mbalimbali isipokuwa yale yanayotuamisha maji na yenye baridi kali.
Amesema Mkonge unapandwa na unavunwa baada ya miaka mitatu na ukianza kuvunwa unavunwa kila baada ya miezi sita kwa muda wa miaka 15.
“Kwahiyo kilimo cha Mkonge ni cha muda mrefu, mtu anaweza kuwekeza kwenye kilimo hichi kwaajili ya kujihakikishia kipato chake cha kujiletea maendeleo na kuhudumia familia,” amsema
Aidha Maghali amesema wapo katika maonesho hayo ya sabasaba kwa ajili ya kutangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye tasnia ya Mkonge ambapo moja ya fursa kubwa waliyonayo ni kilimo hicho cha mkonge.
Amesema wanatangaza fursa hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wakulima wa Mkonge ni wageni ambao wanamiliki mashamba makubwa na wao ndio wamekuwa wakinufaika kwa muda mrefu na kilimo hicho.