NA MWANDISHI WETU,DODOMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali
inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme itakayoboresha
upatikanaji umeme mkoani Songwe ikiwemo ujenzi wa kituo cha umeme na
switching station .
Naibu Waziri Kapinga amesema hayo leo Mei 8 , 2024 bungeni jijini
Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Mbozi, George Mwenisongole
aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo cha upoza Umeme Kakozi,
Tunduma utaanza.
Akijibu swali hilo Kapinga alisema “Serikali kupitia mradi wa
TAZA unaotekelezwa na TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa
kituo cha kupoza umeme cha Nkangamo (Tunduma) kilichopo takribani
kilomita 28 kutoka Kijiji cha Kakozi, Mbozi
Ujenzi wa kituo hiki
unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya
TANESCO na Mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa.”
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa kituo hicho cha Nkangamo (Tunduma)
kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi
na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi.
Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kwa ujumla mkoani Songwe,
Kapinga amesema kuwa mkoa huo unapata umeme kutoka kituo cha Mwakibete kilichopo mkoani Mbeya ambapo laini hiyo ya umeme ni ndefu sana na kupelekea kutokea kwa changamoto za upatikanaji umeme mkoani Songwe.
Kutokana na hilo amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo
ya kujengwa switching station mkoani Songwe pamoja na kituo cha umeme
kitakachojengwa kupitia mradi wa TAZAMA huku uboreshaji wa miundombinu
ya umeme ukiendelea.
Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta aliyetaka
kufahamu ni lini kituo cha umeme cha Uhuru kitakamilika,Kapinga
amesema kituo kipo ukingoni kukamilika na hivyo kuboresha hali ya
umeme wilayani Urambo.