NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi zote za serikali na binafsi zinazohudumia chakula cha zaidi ya watu 100 kuacha kutumia kuni au mkaa badala yake zitumie nishati safi ya gesi.
Ameyasema hayo leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizundua Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupitia 2024-2034 hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema matumizi ya nishati safi yatasaidia nchi kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Aidha Rais Samia ameagiza mikakati ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikishwa kwa wadau wote muhimu kupitia njia rasmi huku akiitaka Wizara ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia mikakati hiyo.
Amesema mkakati huo unapaswa kuwekwa kwenye tovuti yake na kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza ili iwe rahisi kwa wadau kuutumia.
Amesisitiza kuwa wizara zikae na wadau husika serikalini pamoja na sekta binafsi ili kuweza kubaini maeneo ambayo kama yakifanyiwakazi yataongeza kwa haraka upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama himilivu.
Naye Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge duniani, Dk.Tulia Ackson amesema nishati safi ya kupikia italeta manufaa makubwa katika jamii hasa wanawake kwani itawakomboa kiuchumi.
“Wanawake ndio watumiaji wakubwa wa nishati chafu ya kupikia kama mkaa na kuni hivyo wanatumia muda mrefu kwenda kutafuta nishati hizo na kusababisha shughuli za maendeleo kusimama, katika kuliona hilo tayari Bunge limepitisha bajeti ya nishati safi ya kupikia ili wananchi waweze kufikiwanayo kwa urahisi,” amesema Dk. Tulia