NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
FAMILIA ya David Mushi na Mariam Mongi imepinga kukamatwa kwa wanafamilia wake kufuatia mgogoro wa ardhi uliopo Madale, Mtaa wa Scout, Kinondoni, Dar es Salaam, ikisema hatua hiyo imechukuliwa licha ya familia hiyo kuwa na hati za umiliki na hukumu za Mahakama zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 22, 2026, na Mwanasheria wa familia hizo, Wilson Ogunde, familia ya David Mushi na Mariam Mongi inamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 10, ambayo kwa mujibu wa taarifa hiyo ilinunuliwa mwaka 1994 na kusajiliwa kwa hati miliki sita zilizotolewa mwaka 2009.
Ogunde alisema familia hiyo imekuwa ikishiriki katika mchakato wa kutatua mgogoro huo na kwamba hatua za kuwaondoa watu waliokuwa wamekaa katika eneo hilo zilifanyika kwa utekelezaji wa amri ya mahakama kupitia Dalali wa Mahakama na chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi.
Alisema familia hiyo ilipewa ushindi katika mashauri mbalimbali yaliyofikishwa mahakamani, yakiwemo Shauri Na. 286 la mwaka 2016 katika Mahakama ya Rufani na Shauri Na. 316 la mwaka 2010 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2023 Mahakama Kuu katika Shauri Na. 261133 la mwaka 2023 iliamuru familia ya David Mushi irejeshwe katika eneo hilo pamoja na kulipwa fidia ya Sh milioni 80.
Aidha, familia hiyo ilisema Mei 9, 2025, ilipata amri ya kukaza hukumu kupitia Maombi ya Ukazaji wa Hukumu Na. 11992 ya mwaka 2024, huku Dalali wa Mahakama akiteuliwa kwa ajili ya utekelezaji wa amri hiyo.
Ogunde alisema notisi za kuondoka zilianza kutolewa tangu Agosti 2025 na kwamba utekelezaji wa kuwaondoa waliokuwa katika eneo hilo ulifanyika Septemba 3, 2026.
“Si kweli kwamba waliokuwa eneo hilo walivamiwa ghafla na watu wasiojulikana,” alisema Ogunde, akieleza kuwa walipewa notisi zaidi ya mwaka mmoja kabla ya zoezi la kuwaondoa.
Alisema katika kipindi hicho familia za wamiliki zilishiriki katika majadiliano ya kutafuta suluhu yaliyoendeshwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, suluhu ilifikiwa na baadhi ya familia mbili, lakini kwa familia nyingine 12 haikufikiwa baada ya wahusika hao kufungua mashauri mapya mahakamani wakati mchakato wa usuluhishi ukiendelea.
Chanzo cha mgogoro
Akieleza chanzo cha mgogoro huo, Ogunde alidai kuwa Abdallah Kitwanga aliuza vipande vya ardhi hiyo kwa watu wengine wakati kesi ikiwa bado inaendelea mahakamani.
Aidha, alidai Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Gratian Mbelwa, alisaini nyaraka za umiliki kwa wamiliki halali na baadaye akasaini nyaraka nyingine kwa watu walionunua vipande vya eneo hilo.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, hatua hizo ndizo zilizowafanya baadhi ya wananchi kuingia katika hasara wanayoilalamikia.
Familia hiyo imewataka mamlaka za uchunguzi, ikiwemo TAKUKURU na Jeshi la Polisi, kuchunguza madai ya uuzaji wa ardhi hiyo wakati kesi ikiwa mahakamani pamoja na mchakato wa uidhinishaji wa miamala hiyo katika ngazi ya Serikali ya Mtaa.
Kukamatwa kwa wanafamilia
Taarifa hiyo pia imeeleza kuhusu tukio la Septemba 19, 2026, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitembelea eneo hilo na kuzungumza na baadhi ya watu waliokuwa wameondolewa.
Kwa mujibu wa familia hiyo, Mkuu wa Mkoa alitoa agizo la wanafamilia wa Mushi kukamatwa kwa sababu hawakuwepo eneo hilo wakati wa ziara yake na kumuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa kulitekeleza.
Hata hivyo, familia hiyo inasema haikuwa imejulishwa kuhusu ziara hiyo.
Ogunde alisema siku moja kabla ya ziara hiyo, Septemba 18, familia ilikuwa katika kikao cha usuluhishi kilichoongozwa na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi pamoja na wanasheria wake.
Alisema hadi saa 12 jioni familia iliambiwa inaweza kuondoka na kwamba ingejulishwa iwapo ingehitajika, huku Kamishna Msaidizi wa Ardhi akiwa ameeleza kuwa angefika eneo hilo Septemba 19.
Kwa sababu hiyo, alisema baadhi ya wanafamilia wazee walirejea Moshi, wakiwemo waliokuwa wakihitaji matibabu.
Familia hiyo imesema baada ya kupata taarifa za agizo la kukamatwa kupitia mitandao ya kijamii, wanafamilia walirejea Dar es Salaam na kujitokeza kwa hiari kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na kuomba agizo hilo lisitishwe.
Badala yake, kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliagizwa kwenda Kituo cha Polisi Oysterbay na kuwekwa chini ya ulinzi.
Familia imesema waliokamatwa ni bibi wawili na vijana watatu, huku mmoja wa wanawake hao akiwa na umri wa miaka 86 na akihitaji huduma maalumu za afya.
Familia yapinga madai ya kukaidi mamlaka
Familia hiyo imekanusha madai kwamba ilikaidi au kudharau mamlaka, ikisema imekuwa ikihudhuria vikao mbalimbali ilipoitwa na viongozi wa Serikali.
Ogunde alisema familia ilishiriki katika vikao vilivyoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Kamati Maalumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema hatua hizo zilichukuliwa kwa nia ya kuhakikisha wananchi waliokuwa wameingia katika eneo hilo hawapati hasara, licha ya familia hiyo kuwa na msimamo kwamba umiliki wake ulikuwa tayari umethibitishwa na mahakama.
“Familia hizi hazikuwa na sababu yoyote ya kukaidi au kukwepa wito. Ni raia wanaotii sheria na kuheshimu mamlaka,” alisema Ogunde.
Familia hiyo imedai inaamini kuwa Mkuu wa Mkoa alipewa taarifa zisizo sahihi kuhusu kutokuwepo kwa wanafamilia hao wakati wa ziara yake.

