*Awapongeza Wasanii kwa kutopuuza utamaduni wa Mtanzania
*Ampongeza Dk. Samia kwa kuufufua Mfuko wa Utamaduni
*Ataka Wasanii kuhamasisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
NA TERESIA MHAGAMA,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema
Watanzania wana kila sababu ya kulinda utamaduni na utu wao na katu
wasiudhalilishe dhidi ya utamaduni wa kigeni.
Dk. Biteko amesema hayo leo Februari 29, 2024 wakati akimwakilisha
Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa
Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
wadau mbalimbali wa Mfuko huo.
“Kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na
kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi,
kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni
wetu ambao ni mzuri.” amesema Dk. Biteko
Dk. Biteko amewasifu wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa
Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi
zao za sanaa.
Amesema kuwa, wasanii wanao wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai,
kuliondoa kwenye wimbi la kupotea duniani na kuwafanya watanzania
waone lugha yao, tamamduni zao na desturi za Tanzania zinapaswa
kuheshimiwa na kila mtu.
Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kazi ya Sanaa ilikuwa ni kuelimisha na
kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza
ajira na ndio maana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua
kuufufua mfuko huo ambao ulianzishwa mwaka 1992 na ambao ulikuwa
ukisuasua lakini sasa umeimarika.
Dk..Biteko amepongeza wasanii wote ambao wamekuwa wakizingatia vigezo
na mashati ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuwataka
wasanii kuhimizana juu ya umuhimu wa kukopa na kurejesha mikopo ili
iweze kuwanufaisha wengine.
Amesema pamoja na ukweli kwamba sekta ya Utamaduni na Sanaa inaongoza
kwa ukuaji kati ya sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 lakini
bado mchango wake kwa pato la Taifa ni duni kwani inachangia asilimia
0.3 na hii ikimaanisha kuwa Sekta inakua lakini haichangii zaidi.
Ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuweka mazingira
mazuri kwa wasanii ili kukuza sekta ya utamaduni na Sanaa sambamba na
ukuaji wa uchumi.
Vilevile, Dk. Biteko ameitaka Wizara kuwa kiungo cha wasanii na
Serikali hasa katika kazi ambazo wananchi wanapaswa kupata ujumbe au
kuhamasishwa akitolea mfano matumizi ya Nishati safi ya kupikia, afya
na mazingira na kwamba Wasanii hao wanapaswa kupata mapato stahiki.
Aidha, pamoja na kuzipongeza Benki ya NBC na CRDB kwa kuwa wadhamini
na wakopeshaji kwenye suala hilo ametaka Benki zinazotoa mikopo kwa
wasanii hao kulegeza masharti ili wasanii wengi zaidi waweze kupata
mikopo na kuweza kuirejesha kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amewataka Wasanii kutumia kazi zao
za Sanaa kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa utakaofanyika mwaka huu ili wananchi hao waweze kujitokeza kwa
wingi na kuchagua viongozi wanaopenda maendeleo na kuunganisha
wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk.
Damas Ndumbaro amemshukuru Rais, Dk. Samia kwa maono
yake na upendo wake kwa Wasanii nchini ndio maana ameufufua mfuko huo
na kuweka fedha ambazo zinawasaidia wasanii katika kuanzisha,
kuboressha na kupanua shughuli zao za Sanaa.
Amesema kuwa, pamoja na faida mbalimbali za mkopo huo, bado kuna
changamoto kama vile wakopaji kutorejesha mikopo kwa wakati na mfuko
kuwa na chanzo kidogo cha fedha ambapo Wizara inachukua hatua
mbalimbali kushughulikia changamoto hizo.
Amesema kuwa, katika Mfuko huo, itaanziswa sehemu ya kutoa mafunzo
maalum kwa wasanii wachanga ya kuwanoa na kuwawezesha kuunda taasisi
ambayo itakua na itakubalika kwenye benki ili kupata mikopo.
Ameongeza kuwa, Wizara ya hiyo inaangalia sekta ya Sanaa na Utamaduni
kama chanzo cha ajira na uchumi hivyo ameomba wadau mbalimbali kuunga
mkono juhudi hizo za Serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Abdulmajid Nsekela
alisema kuwa, mfuko huo unatoa huduma kuu tatu ambazo ni mikopo ya
masharti nafuu kwa walengwa katika Sekta, kuwajengea uwezo wasanii
kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, urasimishaji, nidhamu
ya biashara na kuwapa nafasi ya kuona fursa mpya zilizopo kwenye
Sekta.
Ameongeza kuwa, katika siku za usoni mfuko unalenga kutoa ruzuku ili
kuwawezesha wajasirimali katika Sekta hiyo.
Viongozi waliohudhuria Mkutano huo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Albert Chalamila, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Utamaduni
Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma.