NA MWANDISHI WETU,KARAGWE
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb) amemuagiza Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kumtafuta na kumchukulia hatua za kisheria Mkandarasi Mohammed Ally wa Kampuni ya Sure Civil and Building Contractors Company Ltd aliyetekeleza ujenzi wa majengo katika Hospitali ya wilaya Karagwe ‘Nyakanongo’ kwa kushindwa kulipa Sh.Milioni 24.7 ya vifaa vya ujenzi alivypokopa kwa mfayabiashara licha ya ujenzi huo kukamilika miaka miwili iliyopita.
Bashungwa ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa Mfanyabiahara huyo, Abineza Ginivian wakati akikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Mji wa Kayanga wilayani Karagwe.
Waziri Bashungwa akiongea kwa njia ya simu na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori amemuagiza kumtafuta Mkandarasi huyo kuhakikisha analipa deni ambalo alikopa kwa mfanyabiashara huyo wakati ujenzi wa hospital ya wilaya Karagwe ukitekelezwa.
“Taaluma ya Ukandarasi hairuhusu Makandarasi wa namna hii wanaodhulumu kwa kuchukua vifaa kwa Wafanyabiashara na kuanza kuwazungusha, sasa huyu Mkandarasi atafutwe alipe deni haraka sana na mchukulie hatua kwa mujibu wa sheria” amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaunga mkono juhudi za vijana wanaojiajiri na haiko tayari kuona juhudi za vijana hao zinakwamishwa na baadhi wa watu waonaowarudisha katika shughuli halali wanazozifanya.
“Hatuchukui hatua kwa Mkandarasi huyu pekee tutawasaka wote wenye tabia kama hizi ambazo zinarudisha nyuma juhudi za vijana waliojiajiri katika sekta ya ujenzi, nimemuagiza Msajili wa Wakandarasi afuatilie ili kubaini wakandarasi ambao ni wajanja kwenye malipo”ameongeza Bashungwa.
Naye, Abineza Ginivian Mfanyabiashara wa vifaa vya Ujenzi ameeleza kuwa baada ya kumkopesha vifaa ya ujenzi Mkandarasi Mohammed Ally wa Kampuni ya Sure Civil and Building Contractors Company Limited amekuwa akimzungusha na kukata mawasiliano na baada ya kumfuata ofisini kwake Dar es salaam alikana deni hilo la Milioni 24.7