NA TERESIA MHAGAMA, TANGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko
amewataka Watendaji katika kampuni inayotekeleza Mradi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhakikisha kuwa, Watanzania
wanapewa kipaumbele katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ikiwemo
ajira na utoaji huduma kama vile ulinzi, chakula, usafiri, bidhaa za
ujenzi, huduma za mawasiliano na huduma nyinginezo ikiwa ni
utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.
Dk Biteko ameyasema mara baada ya kufanya ziara katika kata ya
Chongoleani jijini Tanga na kujionea kazi mbalimbali za ujenzi wa
miundombinu zikiendelea katika eneo hilo ambalo mafuta kutoka nchini
Uganda yatakuwa yakipokelewa na kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri
Kindamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba.
“Serikali inataka kuona watanzania wengi zaidi wanapewa kipaumbele cha
ajira katika hatua zote za mradi na hii inajumuisha kampuni za
Watanzania zinazotoa huduma mbalimbali, kwa kada ambazo ujuzi wake
unapatikana ndani ya nchi, watanzania wapatiwe nafasi na kwa kada
ambazo zinahitaji wataalam wa nje lazima kuwe uwiano wa malipo kati ya
Wazawa na wageni.” amesisitiza Dk Biteko
Kuhusu ujuzi unaotolewa na kampuni ya EACOP kwa watanzania wakiwemo
kutoka vijiji vinavyozunguka mradi, Dk Biteko ameitaka kampuni hiyo
kuhakikisha inatoa ujuzi ambao ni endelevu utakaowawezesha kuendelea
na kazi hata pale mradi utakapokamilika akitolea mfano kuwawezesha
kupata mashine za uchomeleaji ambapo ametaka Halmashauri zishirikiane
na kampuni ili kutekeleza suala hilo.
Akizungumzia utekelezaji mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi litakalokuwa
na urefu wa kilomita 1,443 amesema kuwa, unaendelea vizuri na sasa
umefikia asilimia 32 na mabomba yatakayopitisha mafuta yanaendelea
kuingia nchini kwa ajili ya kuwekewa mifumo ya upashaji joto na
plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba hayo katika
kiwanda kilichopo Sojo wilayani Nzega.
Ameeleza kuwa, ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha mkuza wa bomba
umekamilika, kambi za ujenzi zimekamilika na kazi mbalimbali
zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa gati katika kata ya Chongoleani
mkoani Tanga ambapo meli zitakuwa zikipakia mafuta tayari kwa
kusafirishwa nje ya nchi.
Amesema kuwa, Serikali inayo kiu ya kuwaletea Maendeleo Watanzania na
ikiamua kutekeleza jambo inafanya bila ulegevu wowote, akieleza kuwa,
Tanzania imeshatoa zaidi Dola za Marekani milioni 240 EACOP kama
mwanahisa ambaye ana asilimia 15 kwenye mradi huo na kwamba fedha hizo
zimekuwa zikitolewa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dk.Biteko amekagua eneo mafuta yanapopokelewa
katika bandari ya Tanga na kukagua mita za kupimia mafuta (flow meter)
ambapo aliridhika kuwa mita hizo zinafanya kazi vizuri na hivyo
kuleta ufanisi katika shughuli za upakuaji na upakiaji mafuta katika
Bandari ya Tanga.
Amesema kuwa, baada ya kurekebishwa kwa kanuni za mafuta, Serikali
imeshaagiza mafuta yote ya Ukanda wa Kaskazini yachukuliwe jijini
Tanga pamoja na yale yanayoenda nchi za nje kama vile Kenya na mafuta
ya Ukanda wa Kusini yachukuliwe bandari ya Mtwara.
Kutokana na hilo, ameziagiza Taasisi zinazosimamia mafuta ikiwemo
EWURA, PBPA, TBS na TPA, kufanyia kazi haraka agizo hilo la Serikali
kwani kanuni tayari zilishasainiwa kwa ajili utekelezaji wa suala hilo
ili kuwawezesha watanzania kupata mafuta kwa bei nafuu.
Akiwa jijini Tanga, Dk.Biteko pia ametembelea eneo la hifadhi ya
mafuta ya kampuni ya GBP ambayo inahifadhi mafuta kwa ajili ya
matumizi ya ndani na nje ya nchi na kuwaeleza wawekezaji hao kuwa,
Serikali inathamini uwekezaji huo na ipo tayari kuwaunga mkono katika
mipango yao ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, amemshukuru
Rais, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa kwenye
utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa mradi wa EACOP utakuza pia
mapato ya Mkoa wa Tanga pamoja kipato cha mtu mmoja mmoja.