NA MWANDISHI WETU,LONDON,UINGEREZA
WAZIRI MKUU Dk. Mwigulu Nchemba ameongoza Kongamano la Kimkakati la Uwekezaji na Masoko ya Fedha na kuwaelezea fursa mbalimbali zilizopo Tanzania kupitia DIRA 2050.
Akizungumza na wawekezaji mbalimbali leo (Ijumaa, Oktoba 9, 2026) walioshiriki kikao hicho katika ofisi za Taasisi ya Kimataifa ya Citi zilizopo Stirling Square, jijini London, Uingereza, Waziri Mkuu amesema Serikali imefanya jitihada kubwa ya kupunguza gharama za kuendesha biashara kwa kuandaa mazingira rafiki.
“Tumefanya mengi kupitia uwekezaji wetu binafsi kama vile kuandaa miundombinu ya usafiri wa uhakika ili maeneo mengi nchini yaweze kufikika pindi wawekezaji wanapokuja kuleta mitaji yao,” amesema.
Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa, Waziri Mkuu aliwaeleza jitihada zilizofanywa na Serikali hadi kuifikisha reli hiyo kwenye makao makuu ya nchi. “Mpaka sasa tumekamilisha lots mbili na tunatarajia ndani ya miaka miwili hadi mitatu tutakuwa tumeweza kuunganisha Dar es Salaam na Mwanza,” amesema.
Dktm Mwigulu ambaye yuko Uingereza kwa ziara ya kikazi ya siku tano, aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kwamba Serikali imeanza kuikarabati reli ya TAZARA ili kuufungua ukanda wa Kusini.
Akielezea kuhusu uwepo wa nishati ya kutosha kama kichocheo cha uwekezaji nchini, Waziri Mkuu amesema Tanzania ina umeme wa kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda endapo vitajengwa.
“Hadi kufikia mwaka huu, tumeshafikisha megawati zaidi ya 4,600 ambapo umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji ni asilimia 59, wa gesi asilia ni asilimia 28, nishati ya mafuta ni asilimia 5.8 na nishati ya biomasi ni asilimia 2.9.”
Mapema, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa asilimia kati ya 5.4 hadi 5.9 na kwamba kwa mwaka huu unakadiriwa kufikia asilimia 6.3.
Aliwaeleza washiriki hao kwamba Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kutumia asilimia 74.2 ya sh. trilioni 62.3 za bajeti ya mwaka huu.
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Dk. Juma Malik Akil, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki.






