NA MWANDISHI WETU,BUJUMBURA,BURUNDI
CHUO cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kimepongezwa kwa mchango wake katika kustawisha sekta ya fedha katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia mafunzo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu yanayotolewa na Chuo hicho.
Pongezi hizo zimetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Burundi (BRB), Eduoard Bigendako, alipotembelewa na ujumbe kutoka Chuo cha Benki Kuu unaozuru nchini Burundi kuanzia tarehe 22 hadi 26 Januari 2024, kwa lengo la kuboresha mahusiano na Benki hiyo na sekta ya fedha kwa ujumla pamoja na kutangaza mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Gavana Bigendako alisisitiza kuwa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha BoT yamekuwa nyenzo muhimu ya kuwajengea uwezo watu mbalimbali wenye dhamana ya kuendeleza sekta ya fedha.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa BoT, Kened Nyoni, alimueleza Gavana Bigendako kuwa BoT imeanza rasmi kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba katika utekelezaji wa sera ya fedha nchini .
Aidha, aliongeza kuwa Tanzania kupitia usimamizi wa BoT imepiga hatua katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika mifumo ya malipo na hivyo mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu yatasaidia kuijengea uwezo BRB pamoja na mengine kutatua changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa mifumo ya malipo nchini humo.
Naye mkuu wa chuo cha Benki Kuu, Dk Nicas Yabu, amesema chuo hicho kimekuwa kikipokea washiriki kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Uganda, Kenya, Zimbabwe, Ghana, Zambia, Malawi na Sudani ya Kusini.
Dk. Yabu aliongeza kuwa ushiriki wa mataifa hayo kwenye mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu umetengeneza mazingira mazuri ya kubadilishana uzoefu na kupata suluhu ya changamoto zinazokumba uchumi wa nchi hizo.
Pamoja na kukutana na Uongozi wa Benki Kuu ya Burundi, ujumbe wa BoT unatarajia kukutana na mabenki ya biashara nchini humo kwa ajili ya kutangaza mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.