NA DANSON KAIJAGE,MARA
KIASI cha Sh. Bilioni 3.9 kinatarajiwa kumalizia kulipa fidia ya awamu ya pili kwa wananchi 49 waliopisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Oktoba 10 , 2023 nkoani hapa na kueleza kuwa tayari kiasi hicho kimewasilishwa Wizarani mwezi Agosti mwaka huu.
Amesema kiasi hicho cha fedha lengo kubwa ni kuendelea kulipa wananchi hao waliobakia baada wananchi 85 kulipwa fidia zaidi ya Bilioni 4 katika awamu ya kwanza.
Bashungwa amempongeza Mbunge wa Musoma mjini, Vedasto Mathayo kwa kuendelea kufuatilia kwa karibu mradi wa ujenzi wa Kiwanja hicho pamoja na fidia kwa wananchi hao.
“Mheshimiwa Mbunge Vedasto umekuwa mkali sana juu ya fidia kwa wananchi wako na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari amesikia kilio chako, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha tunamaliza suala hili angalau kwa awamu ili tulikamilishe”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inalipa madeni ya Mkandarasi kwa wakati ili kuwaweza kuendelea na kazi kwa kuongeza kasi ya ujenzi na kukamilisha kwa viwango bora kama ilivyo kwenye mkataba.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan niwahakikishie kuwa baada ya ziara yangu, mimi na timu yangu tutajipanga kumlipa Mkandarasi kwa awamu ili asitoke eneo la mradi mpaka uwanja ukamilike na ukabidhiwe kwa wana Mara”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuufungua Mkoa wa Mara kupitia miundombinu ya barabara ambapo mtandao wa barabara kutoka Butiama- Serengeti- Nata- Mugumu- Nyamongo- Tarime na kurudi Musoma mjini ipo kwenye kipaumbele kikubwa cha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Kiwanja hicho, Mkurungenzi wa Miradi TANROADS, mhandisi Boniface Mkumbo amesema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania kwa asilimia 100 na hadi sasa ujenzi umefikia asiliamia 52 na umetoa ajira 165 kati ya ajira hizo ajira 147 ni Watanzania.
Amesema kwamba kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma kutarahisisha huduma za usafiri wa anga na kukuza sekta ya utalii mkoani Mara kwani kiwanja hicho ni kiunganishi cha mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.