NA DANSON KAIJAGE,DODOMA.
HOSPITALI ya Benjamini Mkapa(BMH) inatarajia kuanzia Oktoba 16, 2023 kuanza kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watu wazima kwa njia ya kufungua au kutofungua kifua hali itakayosaidia kuokoa idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wanapoteza maisha.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 10, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk.Alphonce Chandika Jijini Dodoma wakati wa kuelekea maadhimisho ya miaka nane ya utoaji huduma kwa wateja katika hospitali hiyo pamoja na kupokea tuzo ya Daktari bora wa upandikizaji uloto.
“Hivi karibuni tunaenda kuanzisha huduma za upasuaji wa moyo kwa watu wazima siku za nyuma mlikuwa mkisikia kambi ya upasuaji wa moyo ilikuwa ikishughulika na watoto kwahiyo safari hii tunaenda kuongeza huduma twende na kwa watu wazima
“Tatizo la moyo kwa watu wazima lipo, tumekuwa tukiwapa rufaa wagonjwa kwenda JKCI ambapo tulikuwa tunawaongezea msongamano, lakini na sisi kama Hospitali ya Benjamin tunaenda kushirikiana na wadau kutoka nchi za nje lakini pia Jakaya Kikwete tushirikiane kwa pamoja kuanzisha huduma hizo hapa”ameeleza Dk.Chandika.
Katika hatua nyingine Dk. Chandika amesema kuwa kwa kipindi cha miaka nane ya utendaji wameweza kutoa huduma mbalimbali za kibingwa na bobezi kwa mafanikio makubwa.
Awali Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk. Stella Malangahe ametumia fursa hiyo kuelezea namna walivyojipanga katika kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kikamilifu.
“Kipekee nimshukuru sana Mungu Safari ilikuwa ni kubwa nilipoanza mpaka hapa nilipofika naushukuru sana uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa namshukuru Mkurugenzi wetu pia wao wamekuwa mstari wa mbele kuniwezesha mimi na wenzangu kufanya kazi zetu kwa ufanisi zaidi na ninaahidi kuwa timu yangu ya upandikazaji uroto nitaendelea kufanya nao kazi kwa bidii zaidi kwa kadri Mungu atakavyozidi kutuongoza” amesema.
Sambamba na hayo Dk Malangahe ambaye ni daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu ameibuka mshindi wa nne miongoni mwa madaktari bingwa wote nchini katika tukio lililofanyika Oktoba 4 jijini Dar es salaam lililoratibitiwa na Tanzania Health Summit.