NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATU 604 wamepata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Hoapitali ya Dar Group Dk. Tulizo Shemu alisema upimaji huo ulifanyika kwa muda wa siku mbili ambapo wananchi walipata huduma na upimaji, ushauri pamoja na kupewa dawa kwa wale waliokutwa na matatizo.
Dk. Shemu alisema mwitikio wa wananchi ulikuwa ni mkubwa na kuwaomba wananchi wakati mwingine watakaposikia kuna upimaji wa magonjwa mbalimbali unafanyika mahali wasiache kwenda kupima afya zao.
”Watu 604 walifanyiwa vipimo vya awali vya magonjwa ya moyo kati ya hao 99 walifanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo na 58 tumewakuta na matatizo ya moyo yanayohitaji matibabu ya kibingwa tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”,.
“Wagonjwa wengi tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu na wengine wameshapata madhara ya shinikizo la damu hii ikiwa ni pamoja na kutanuka kwa misuli ya moyo, wengine mishipa yao ya damu ya moyo imeziba, kuna ambao tumewakuta na kiwango kikubwa cha mafuta kwenye damu pamoja na matatizo mengine ya moyo”, alisema Dk. Shemu.
Dk. Shemu alisema gharama za matibabu ya moyo ni kubwa na kwa asilimia 80 magonjwa hayo yanaweza kuepukika njia moja wapo ya kuyaepuka ni kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara ili kujua kama unamatatizo ya moyo na kuanza matibabu mapema kuliko kusubiri wakati ambao mioyo umepata shida na kuanza matibabu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mobhare Matinyi ambaye aliongoza matembezi ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza alisema wilaya hiyo imejipanga kuhamasisha jamii kufanya mazoezi na kupima afya ikiwa ni njia moja wapo ya kupambana na magonjwa hayo yakiwemo ya moyo.
“Leo hii vikundi mbalimbali vya mazoezi vimetembea umbali wa KM 4 kutoka uwanja wa Uhuru hadi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hospitali ya Dar Group kwa ajili ya kufanya mazoezi. Ninaipongeza JKCI kwa kusherehekea siku ya moyo duniani kwa kufanya upimaji wa afya na kuandaa matembezi haya”,.
“Licha ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi Wilaya ya Temeke pia inahamasisha wananchi kufanya usafi katika mazingira yao, kupima afya pia katika matukio makubwa yanayofanyika tunawahamasisha wananchi kuchangia damu na mwitikio huwa ni mkubwa”, alisema Matinyi.
Mkuu wa Wilaya huyo alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha katika sekta ya afya ambapo sasa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inauwezo wa kuwahudumia watanzania na wagonjwa kutoka nje ya nchi na kuwaomba wananchi waitumie hospitali hiyo katika matibabu.
Nao wananchi walioshiriki zoezi la upimaji na matibabu hayo ambayo yalienda sambamba na matembezi ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kusema imewasaidia kupata elimu na matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Mimi ninashida ya presha nilisikia katika taarifa ya habari kutakuwa na huduma ya upimaji nami nikaamua kuja kupima ili nione maendeleo ya afya yangu, nashukuru sana nimepima na nimepewa dawa za kutumia huduma hii nimeipata bila malipo yoyote yale”,
“Huduma niliyoipata ni nzuri, ninaomba huduma hii iweze kwenda hadi vijijini ili wananchi wengi wanaoteseka na magonjwa ya shinikizo la damu na moyo ambao uwezo wao kifedha ni mdogo waweze kufaidika nayo”, alishukuru Christina Mohamed mkazi wa Gongo la Mboto.
“Mimi sina bima ya afya nilikuja na mama yangu kupima afya namshukuru Mungu sina tatizo lolote lile la moyo ila nimekutwa na matatizo mengine nimepewa dawa za kikohozi na mafua , ninawashauri wananchi wenzangu nao waje kupima afya zao kwani huduma inatolewa bila malipo yoyote yale”, alisema Emmanuel Babu mkazi wa Tabata.