NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Holence Rwazo amefariki dunia wakati akiogelea katika chemchem ya maji moto iliyopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, lilitokea juni 24, mwaka huu, wakati mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Masoko na Ujasiriamali, akiogelea kwenye chemchem hiyo na kwamba chanzo cha tukio hilo ni marehemu kuzidiwa na maji wakati akiogelea.
“Juni 24, saa 6:00 mchana huko Kijiji cha Chemka Kata ya Masama Rundugai, Hassan Fumbwee mkazi wa Njiapanda ya KCMC aligundua kufariki kwa rafiki yake Holence Rwazo mwanafunzi wa Chuo cha Ushirika Moshi kozi ya masoko na ujasiriamali mwaka wa tatu wakati wakiogelea kwenye chemchem ya maji moto Chemka,” amesema.