NA MWANDISHI WETU
Nahodha wa klabu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Mohamed Hussein (Tshabalala) amezua mjadala baada ya kuenea kwa taarifa kuwa amekataa kujiunga na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kaizer ambao ni miamba ya soka Afrika Kusini ilimuwekea Tshabalala dau la usajili la Tsh. Milioni 400 na Mshahara wa Tsh. Milioni 30 ili ajiunge nao lakini mlinzi huyo wa Wekundu wa Msimbazi alipiga chini ofa hiyo.
Tshabalala ambaye mkataba wake na klabu ya Simba ulikuwa uishe baada ya kumalizika Ligi ya Soka Tanzania Bara siku chache zijazo, ametia Saini ya kuitumikia Simba miaka mitatu kwa ada ya usajili ya Tsh. Milioni 300 (pungufu ya Milioni 100 ukilinganisha na ya Kaizer Chiefs) na mshahara wa Tsh. Milioni 10 kwa mwezi (pungufu ya Milioni 20,000 ya Kaizer Chiefs).
Demokrasia lilifanya kikokotoo cha kuangalia gharama ya fursa (opportunity cost) ya kuacha kusajili Kaizer Chiefs yenye mshahara mnono na dau kubwa la usajili na kuamua kuchukua mshahara wa 1/3 tu na mkataba wa pungufu ya Milioni 100.
Hesabu ni kwamba kwa kukataa kujiunga Kaizer Chiefs, Tshabalala anapoteza milioni 20 kwa mwezi, milioni 240 kwa mwaka ambazo ni sawa na Milioni 720 kwa miaka mitatu.
Na kukataa mkataba wa milioni 400 na kukubali wa milioni 300, mlinzi huyo amepoteza milioni 100 hivyo jumla Tshabalala atapoteza Milioni 820 kwa miaka mitatu kwa kucheza Simba na kuitosa Kaizer Chiefs.
KWANINI ALIFANYA MAAMUZI HAYO?
Uchunguzi wetu umeona wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa wakikataa kutoka nje ya nchi kutafuta Maisha bora na uzoefu wakibweteka na sifa na ‘mizinga’ Pamoja na ofa kutoka kwa mashabiki na viongozi wa klabu.
Lingine linalowafanya wasiondoke nchini ni kuogopa kusugua benchi kwenye vilabu vya nje ya nchi kitu ambacho kama mchezaji ana ari ya kupambana, hawezi kuathirika na hoja hii.
Makato ya kodi na Maisha ya juu nje ya nchi ni hoja nyingine ambay0 labda ilipelekea Tshabalala kuamua kusalia nchini, lakini hesabu zinaonesha kwa miaka mitatu aliyopewa na Kaizer Chiefs, milioni 820, bado zisingekwisha zote hata kama kodi na Maisha ya Afrika kusini yapo juu Zaidi ya Tanzania.
Sababu hizo hapo juu zimewafelisha wachezaji wengi wa Tanzania kubaki nchini na kupiga chini ofa za vilabu vya nje.
Wachache waliothubutu na kufanikiwa ni Pamoja na Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu Simon Msuva.