NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
MKUTANO mkuu wa 28 wa mwaka, wanahisa wa Benki ya CRDB umeidhinisha mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi ya kulipa gawiwo la Sh. 45 kwa kila hisa hivyo kufanya jumla ya gawiwo kwa mwaka wa fedha 2022 kuwa Sh.Bilioni 117.5
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika katika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) jana huku wengine wakifuatilia ajenda zilizojadiliwa kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dk Ally Laay alisema gawiwo lililopitishwa ni sawa na ongezeko la asilimia 25 likilinganishwa na gawiwo la Sh. 36 kwa hisa lililolipwa mwaka jana hali inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa pato kwa hisa ambalo mwaka 2022 limefika Sh. 134.5.
“Kwa mara nyingine tena, tunafurahi kupata matokeo mazuri kwa mwaka 2022 yaliyochangia kuongeza thamani kwa wanahisa wetu. Faida tuliyoipata mwaka 2022 ni uthibitisho wa utekelezaji makini wa mpango mkakati wetu wa miaka mitano wa 2018 hadi 2022. Benki ilipata faida ya baada ya kodi ya Sh.Bilioni 351.4 sawa na ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na Sh.Bilioni 268.2 za mwaka 2021,” alisema Dk Laay.
Vilevile, Dk Laay alisema kampuni tanzu ya Burundi nayo inazidi kuimarika hivyo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye faida ya kampuni mama.
Alieleza kuwa, Kwa mwaka 2022, Benki ya CRDB Burundi imepata faida kubwa zaidi tangu lilipoanzishwa mwaka 2012.
Kampuni hiyo tanzu ilipata faida ya Sh.Bilioni 23 mwaka 2022 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 79.7 kutoka Sh.Bilioni 12.8 iliyopatikana mwaka 2021.
Akizungumzia utendaji wa Benki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema katika mwaka wa fedha 2022, waliendeleza juhudi za kukuza mapato na wakafanikiwa kwa kiasi kizuri kwani mapato ya uendeshaji yaliongezeka kwa asilimia 28 na kufika Sh.Bilioni 745.8 yakichangiwa na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa.
Kwa mwaka 2022, uwiano wa mikopo chechefu ulishuka hadi asilimia 2.8 hivyo kuwa ndani ya ukomo uliowekwa kikanuni wa kutozidi asilimia 5
Mizania ya Benki pia, amesema ilikua kwa asilimia 32 kutoka Sh.Trilioni 8.8 mwaka 2021 hadi Sh.Trilioni 11.6 hivyo kuwa taasisi ya kwanza ya fedha nchini kuvuka Sh.Trilioni 10 .
Ongezeko hilo, alisema limechangiwa na kuimarika kwa amana za wateja zilizoongezeka kwa asilimia 26.4 na kufika Sh.Trilioni 8.2 kutoka Sh.Trilioni 6.5 za mwaka 2021.
Nsekela alisema ufanisi uliopatikana umewezesha kuwekeza zaidi kuimarisha huduma kwa kuwekeza kwenye majukwaa ya kidijitali ambayo yanasaidia kukidhi mahitaji ya wateja kwa kuwapa huduma wazitakazo mahali walipo na kuzitumia kwa namna waitakayo.
Nsekela amewashukuru wanahisa wa Benki hiyo kwa ushirikiano ambao wameendelea kuipatia menejimenti na wafanyakazi wa benki hiyo, na kuwawathibitishia kwamba Benki itaendelea kufanya vizuri ili kuwapa thamani ya uwekezaji walioufanya na wanaoendelea kuufanya.
Katika hatua nyingine wanahisa hao waliwachagua kwa mara nyingine tena Profesa Neema Morina na Miranda Mpogolo kuwa Wajumbe Huru wa Bodi ya Wakurugenzi.
Akizungumzia gawiwo lililoidhinishwa, Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Benki ya CRDB ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vunjo, Dk.Charles Kimei alisema wanahisa wamefurahia ongezeko la gawiwo lililopendekezwa.