NA MUNIR SHEMWETA, WANMM
WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na ile ya Makaazi Zanzibar pamoja na Taasisi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na lile la Zanzibar (ZHC) zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya ardhi na Nyumba.
Hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa mwongozo wa ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Ofisi ya Makamu wa Pili SMZ kuhusu taasisi zisizo za muungano kukutana na kubadilishana uzoefu wa utendaji wa majukumu yao na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji majukumu yao.
Utiaji saini makubaliano hayo ya pande hizo ulifanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Anthony Sanga na yule wa Makazi Zanzibar Dk Mngereza Miraji wakati Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) likiwakilishwa na Mkurugenzi wake Hamad Abdalah na lile la ZHC Mwanaisha Said mbele ya Mawaziri wa wizara hizo Dk Angeline Mabula na Rahma Ali
Maeneo yanayokwenda kutekelezwa katika ushirikiano huo ni kukusanya, kuchakata na kubadilishana taarifa za ardhi baharini, kubadilishana uzoefu kwenye maendeleo na matumizi ya mifumo ya habari na teknolojia kwa sekta ya ardhi pamoja na kuandaa na kutekeleza sera, sheria na miongozo mbalimbali ya sekta ya ardhi .
Maeneo mengine ni kushirikiana kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika mfumo wa usimamizi na maendeleo ya sekta ya milki kuu inayojumuisha makaazi na nyumba, utafiti na maendeleo kwenye sekta ya ardhi, utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika usimamizi na maendeleo ya mji Mkongwe.
Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini makubaliano hayo yaliyofanyika jijini Dodoma Mei 20 , 2023, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Mabula alisema, makubaliano yaliyofikiwa yaingie katika utekelezaji nay awe fursa kwa kwa kila mmoja kuona namna ya kuboresha mahusiano katika sekta ya ardhi kwa kuwa, upande wa Tanzania Bara sekta ya ardhi ni wezeshi na inapofanya vibaya inakwaza sekta nyingine.
Kwa mujibu wa Dk Mabula, changamoto anayoina ni kuwa makubaliano hayo yamechelewa sana kutokana na kila upande kuwa na mambo mazuri iliyofanya na kusisitiza ushirikiano huo utakuwa njia bora za kutatua migogoro lakini pia kuleta salama ya milki, ufanisi na kikubwa kuona namna ya kuisimamia sekta ya ardhi.
‘’Msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ni sekta ya ardhi kuwa kinara katika kuongoza na kuifanya ardhi kupangika vizuri na kuleta manufaa kwa wananchi. Sekta hii inaleta maisha bora na hatuwezi kuwa na maisha bora wakati kila siku kuna migogoro na hatuwezi kutoa fursa watu wawekeze’’ alisema Dk Mabula
Ametaka makubaliano yaliyofikiwa yasimamiwe kwa vitendo sambamba na kuwa na vikao vya mara kwa mara vya ufuatiliaji na tathmini katika kutekeleza makubalinao.
Ametoa rai kwa makatibu wakuu kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa kuwekewa utaratibu mahsusi sambamba na kusimamiwa kwa kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kujua kinachoendelea.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar Ally amesema, katika utekelezaji wa makubainao ipo haja kwa wataalamu kuweka mpango kazi utakaoainisha vitu vya kuanza navyo na iwapo zipo changamoto basi ziwasilishwe kwa mawaziri kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Amesema, makubaliano yaliyosainiwa yakifanikishwa serikali zote mbili za SMT na SMS zitakuwa zimepiga hatua kubwa sana na kuwafanya viongozi wake kuwa salama kwa kuwa wizara hizo zinahudumia na kutoa huduma bora kwa wananchi.
‘’Katika makubaliano haya sote tunabadilishana uzoefu lakini wenzetu mmetuzidi mtuone kama watoto, sisi tuna yetu na ninyi mna yenu ila mmetuzidi kwa hiyo tutakuwa tunahitaji msaada zaidi kwenu kuliko sisi’’ alisema Ally.