NA MWANDISHI WETU, IRINGA
KAMPUNI ya Barrick Gold Corporation imedhamini na kushiriki katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na taasisi ya kuchipua na kuendeleza vipaji vya uongozi kwa vijana (AIESEC Tanzania) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Iringa na kuwashirikisha wanafunzi,wahadhiri na wadau mbalimbali.
Kupitia kongamano hili ambalo hufanyika kila mwaka, wanafunzi huweza kufahamu jinsi taasisi mbalimbali nchini zinavyoendesha shughuli zake lengo kubwa ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kujua vipaji walivyonavyo, kujifunza jinsi ya kujiamini na kukabiliana na ushindani katika soko la ajira, kujitambua uwezo wao ni jinsi gani wanaweza kushiriki kutoa mchango wa kuendeleza taifa pindi wamalizapo masomo yao.
Maofisa Rasilimali Watu Waandamizi wa Barrick pia walishiriki katika maonesho na kongamano hilo ambapo walipata fursa kuzungumza na wanafunzi kuhusiana na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajira,kuendeleza vipaji vyao pia wanafunzi walipata fursa kuelewa jinsi kampuni ya kimataifa ya Barrick, inavyoendesha shuguli zake kwa kutoa kipaumbele kusaidia jamii sambamba na mpango wake wa kuibua na ukuzaji wa vipaji kwa vijana wa kitanzania na wafanyakazi wake.