NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
HALMASHAURI ya mji Kibaha mkoani Pwani imetumia kiasi cha shilingi bilioni 3.9 katika kutekeleza miradi 12 ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya,elimu,miundombinu ya barabara,pamoja na mambo mengine ya huduma za kijamii.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon wakati alipokuwa akitoa taarifa ya miradi ambayo itatembelewa katika mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023.
Mkuu huyo aliongeza kuwa , Mwenge huo utaweza kupita katika miradi mbali mbali ambapo baadhi yao itawekewa mawe ya msingi,pamoja na kuzinduliwa.
“Katika halmashauri ya Kibaha mji tumetembelea miradi yapatayo 12 ya maendeleo ambayo jumla yake imegharimu shilingi bilioni 3.9 ambapo fedha nyingine kati ya hizo zimetoka kwa wadau wengine wa maendeleo,”amesema
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kibaha Mji Mshamu Munde amesema kwamba miradi ambayo wameianzisha watahakikisha kwamba wanailinda na kuitunza kwa hali na mali kwa lengo la kuwasaidia wananchi.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Kaim ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuweza kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo ambayo imegusa maslahi ya wananchi kwa ujumla.
Pia ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kuulaki Mwenge wa Uhuru mwaka huu kwani unakuja kuangazia maendeleo yanayoendelea kutamalaki kwenye Halmashauri za Mkoa wa Pwani ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Mwenge wa Uhuru umeweza kukimbizwa katika Halmashauri ya Mji Kibaha katika sekta mbali mbali ikiwemo,afya,elimu,miundombinu ya barabara,maji,mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na malaria