NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala iko mbioni kuanza kutoa huduma mpya ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo. Huduma hii inatarajia kuanza kutolewa baada ya Bohari ya Dawa (MSD) kukamilisha hatua za mwisho za ufungaji mashine za kisasa 10 za kusafisha damu.
Ufungaji wa mashine hizi ni muendelezo wa maboresho ya huduma za afya nchini yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk.Irene Kato ameishukuru Serikali kupitia MSD kwa kufunga mashine za kisasa kwenye hospitali hiyo ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo itawapunguzia wahitaji wa huduma hiyo kuifuata mbali.
Kabla ya kukabidhiwa mashine hizi kwa Hospitali husika MSD kwa kushirikiana na Wataalam wengine watatoa mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali hiyo na kuendelea kuhakikisha vitendanishi vya mashine hizo vinapatikana wakati wote ili kuepuka kukwamisha huduma.