NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka jamii ishirikiane na akinamama katika malezi ili kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania.
Ametoa wito huo jana usiku (Jumapili, Mei 14, 2023) wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya Mtoko wa Mama kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani. Hafla hiyo iliandaliwa na taasisi ya Binti Lindi Initiative.
“Akinababa washirikiane na akinamama katika malezi ya watoto kwani kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tumelelewa na akinamama zaidi, lakini akinababa tunapaswa vilevile kujipa muda na kufuatilia mwenendo wa tabia ya mtoto kuanzia asubuhi mpaka usiku,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa jamii kuheshimu na kuthamini mchango wa mama katika malezi. “Kama wahenga walivyosema, kuzaa siyo kazi ila kazi ni kulea mwana, tushirikiane na akinamama wote katika malezi ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania,” amesema.
“Ninatambua kuwa mama zetu katika karne hii mnafanya shughuli nyingi za kiuchumi kwa ajili ya ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla. Niwasihi sana muendelee kuwa vinara katika suala la malezi ya watoto,” amesisitiza.
Amewataka wazazi na walezi wajitambue kuwa wao ni taasisi muhimu tena ya kwanza katika malezi ya mtoto. “Timizeni wajibu wenu, shirikianeni na taasisi za kiserikali ili kukuza na kuimarisha maadili kwa watoto wenu pamoja na kutenga muda wa kuwafuatilia ili kujua changamoto zao na kuwelea ipasavyo.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Mwanaidi Ali Khamisi alisema Siku ya Mama Duniani huadhimishwa kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei kila mwaka.
Alisema kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto na wizara yake iliamua kuunda madawati ya watoto kwenye shule zote za msingi na sekondari ili wapate mahali pa kujieleza pindi wakiona dalili ama wakifanyiwa ukatili.
“Hadi kufikia Machi 2023, madawati 1,488 yameundwa ambapo 1,070 yako kwenye shule za msingi na 418 yako kwenye shule za sekondari. Lengo letu ni kuzifikia shule 25,000 hapa nchini,” alisema.
Wakati huohuo, jopo la washiriki wa mjadala kuhusu malezi na maadili walisema kuwa maadili ya mtoto yanaanzia kwenye ngazi ya utoto na kusisitiza kwamba maadili yanapaswa yafundishwe kuanzia nyumbani na kisha shuleni.
Kwa nyakati tofauti, walisisitiza kuwa suala la lishe bora kwa watoto katika ngazi zote za makuzi kuwa ni la muhimu. “Lishe isipokuwa kamili kwa mtoto, inaweza kuleta ulemavu hata kama alizaliwa akiwa mzima (bila ulemavu),” alisema Bi Sophia Mbeyele ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Makumbusho ambaye amekuwa akifanya harakati kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Mhariri wa CLOUDS na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuuelimisha umma kuhusu maadili na malezi kupitia makala na vipindi maalum ambavyo vitalenga kukabiliana na changamoto za watoto za wakati huu.
Washiriki wengine katika jopo hilo walikuwa ni Sadaka Gandi ambaye ni mtaalamu wa mausla ya saikolojia; Dk Filbert Komu (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na Mathias Haule (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum).
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya Binti Lindi Initiative, Kija Yunus alisema: “Niwasihi vijana tuwaheshimu wazazi wetu na kamwe tusiwaone kuwa wamepitwa na wakati kwani sikio halizidi kichwa. Tuepuke vishawishi vya fedha vinavyoweza kuwa chanzo cha kuleta tatizo la kimaadili miongoni mwetu,” alisema.
Akitoa maoni ya viongozi wa dini, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad, alisisitiza agizo la Mwenyezi Mungu kwa wanadamu linalotaka wanadamu kuwaheshimu mama zao kwani walipitia changamoto nyingi kuanzia ujauzito hadi makuzi, changamoto ambazo watoto hawawezi kuzijua.
Akisisitiza kuhusu malezi, Sheikh Alhad alisema: “Mtoto anapaswa anyonyeshwe maziwa ya mama yake kwa miaka miwili ili kumjengea hatma nzuri na kuimarisha uhusiano na mama yake na muumba wake. Mtoto asiyenyonya kwa miaka miwili hukosa mahusiano na Mungu,” alisisitiza.
Naye, Askofu Sylvester Gamanywa wa Kanisa la BCIC la jijini Dar es Salaam aliomba viongozi wa dini washirikishwe kwenye suala la maadili ili kujenga hofu ya Mungu. “Bila hofu ya Mungu, sheria haifanyi kazi. Na hofu hii ya Mungu inatoka kwenye misahafu yetu, Niwasihi viongozi wa dini tusiishie kusalisha tu, bali tujenge hofu ya Mungu ndani ya jamii,” alisisitiza.
Halfa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, mabalozi na wanawake na mabinti kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.