NA MWANDISHI WETU, MTWARA
WAKULIMA wa mihogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara wameishukuru Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) Kituo cha Naliendele kwa kuwashirikisha katika kutafiti mbegu bora za zao la Mihogo Wilayani humu.
Utafiti huo umefanyika kupitia mashamba darasa ambayo
yalianzishwa na kituo hicho (TARI Naliendele) katika maeneo ya wakulima kwa lengo la kutafiti mbegu bora kwa pamoja na wakulima wa eneo husika.
“Kwanza kabisa sisi wakulima tumepata fursa nzuri ya kujifunza uhalisia kwa vitendo na kutambua ubora wa mbegu sisi wenyewe, huu mpango ni mzuri kuliko ule wa kuletewa mbegu na kuambiwa ni mbegu bora bila kujua ubora wake upo wapi,” amesema Bakari Fredy Mkulima wa zao la Mihogo Kata ya Mkunwa Halmashauri ya Mtwara.
Bahati Abeid mkulima wa mihogo amesema utafiti huo umewasaidia wakulima kutambua namna bora ya kupanda mbegu bora na kuhakikisha inaleta tija katika uzalishaji.
“Katika utafiti huu, nimejifunza kwanza namna ya kutambua mbegu bora, hapa kulikuwa na mbegu nyingi, zimepandwa kwa pamoja na tumeziona zinakuwa na leo tunavuna na katika kuvuna tumefanya ulinganisho kwenye masuala mbalimbali kama magonjwa, uzaaji , na ladha , ujazo na hii imetupa nafasi sasa kuamua aina ya mbegu ambayo tunaweza kulima wenyewe na ikaleta tija,” amesema.
Afisa Kilimo Kata ya Mkunwa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Musa Liponda amesema ushirikishwaji wa wakulima katika kutafiti mbegu bora umewawezesha wakulima kubadili fikra katika kilimo cha Mihogo.
“Hii njia imekuwa ya tija na imeleta fikra nyingine Kwa wakulima , wamefanya wenyewe na wameona utofauti Kati ya mbegu za asili na hizi mbegu bora ambazo zimeletwa na TARI Naliendele,” amesema.
Mtafiti wa Mazao Jamii ya Mihogo na Viazi kutoka kituo cha TARI Naliendele Festo Masisila amesema kituo hicho kilianzisha na kupanda mbegu bora zaidi ya aina tisa katika mashamba darasa maeneo mbalimbali ikiwemo Mkunwa kwa lengo la kuwawezesha wakulima kujifunza namna mbegu hizo mpya zinavyofanya katika uzaaji na kuvumilia magonjwa
Alizitaja mbegu hizo kuwa ni TARICASSA 1,2,3,4,5, aina nyingine ni mbegu ya Mkuranga, Chereko, Kiroba , Kipusa na Mkumba.
Mtafiti huyo amesema kila mbegu ina sifa yake na kwamba mojawapo ya sifa hizo ni kukomaa haraka, uzaaji kwa wingi, muonekano kwa ajili ya kuuzwa sokoni.
Masisila amesema TARI walifanya utafiti na wakulima kwa pamoja ili wakulima wenyewe waone mahitaji yao katika kilimo cha zao la Mihogo na kufanya maamuzi sahihi ya kuleta tija katika kilimo cha mihogo nchini.
Mtafiti huyo amesema mbegu hizo ni mbegu bora ambazo zinavumilia magonjwa na kuzaa kwa wingi ikilinganishwa na mbegu za asili huku akiwataka watendaji katika Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mbegu bora kusaidia wakulima kuwa na kilimo chenye tija kwenye uzalishaji wa zao la Mihogo nchini.
Masisila amesema mbegu hizo bora zina uwezo wa kuzaa mara tatu zaidi kulinganisha na mbegu za asili.
“Katika hizo mbegu bora ambazo tumefanya tathmini yake na wakulima, mbegu ya chini inazaa tani 22 kwa hekari 2.5 lakini mbegu za asili inazaa tani nane kwa hekari hiyo hiyo 2.5,” amesema.
Amesema katika mbegu hizo bora zipo ambazo zinazaa zaidi ya tani 40 huku akiitaja mbegu ya Mkumba ambayo inazaa hadi tani 50 Kwa hekari 2.5.
Masisila amesisitiza wakulima kuendelea kutumia mbegu bora za Mihogo ili kuwatoa wakulima katika uzalishaji duni na kwenda kwenye uzalishaji wenye tija.
Kwa mujibu wa takwaimu katika Wizara ya Kilimo inaonyesha kuwa mwaka 2017/18 Tanzania ilizalisha kiasi cha tani milioni 8.4 cha zao la Mihogo.
Masisila amesema endapo Halmashauri watawekeza katika kilimo cha kutumia mbegu bora za Mihogo, uzalishaji utaongezeka zaidi