NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya NMB imekamilisha awamu ya kwanza ya ukarabati wa jengo la wazazi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Ukarabati huo umegharimu Sh. milioni 250 zilizogharamia matengenezo wodi ya uzazi na kuikabidhi kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu mwishoni mwa juma lililopita.
Katika hafla ya makabidhiano Ummy alishuhudia pia kusainiwa makubaliano ya ukarabati na utunzaji wa jengo hilo.
Makubaliano hayo ya miaka mitatu na ufadhili yamewezesha jengo hilo kupewa jina jipya Jengo la Uzazi la NMB.
Katika ushirikiano huo, NMB pia inaisaidia mchakato wa kutunza taarifa za kitengo hicho kidijiti zikiwemo kumbukumbu za matibabu.
“Nimetaarifiwa kuwa Benki ya NMB imeanza kufanyia marekebisho majengo ya Taasisi ya Mifupa – MOI. Tunawashukuru sana na kuwapongeza kwa kuja na mpango huu wenye tija kubwa katika uimarishaji wa utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na vituo vingine vya afya nchini,” amesema Ummy.
Vilevile NMB imechangia vifaa tiba kwa ajili ya wodi hiyo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema ni vitanda vya kujifungulia akina mama vya kisasa zaidi vinavyotumia umeme vyenye thamani ya Sh milioni 50.
Ummy alisema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya kitaifa.
“Kipekee kabisa niwapongeze NMB kwa ushirikiano endelevu baina yenu na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya afya. Kwa miaka yote 25 ya utoaji huduma kwa Watanzania, mmekuwa mstari wa mbele kusapoti ustawi wa maendeleo yao kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, hivyo kusaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa letu kwa ujumla.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo sekta ya afya ni kipaumbele chake kikuu, inaendelea na jitihada mbalimbali za kupunguza vifo vya kinamama na watoto. Hii ni changamoto kubwa ambayo tunapaswa kuikabili kwa kuzingatia mipango bora na elimu sahihi na ya kina ya afya ya uzazi,” alisisitiza Waziri Ummy.
Zaipuna aliishukuru serikali na menejimenti ya MNH kwa kuipa NMB nafasi ya kuwa mbia wa hospitali hiyo.
“Wazazi watakaojifungua katika Jengo la Uzazi la NMB, watapewa maarifa na elimu ya kuweka akiba kwa ajili ya watoto wao pindi watakapozaliwa. Pia wazazi wote watapewa kifurushi cha zawadi kutoka NMB chenye kadi ya pongezi, nguo maalum ya kupimia uzito wa mtoto atapopelekwa kliniki, kipima joto na zawadi nyinginezo,” amesema.
Zaipuna alisema kila mwaka wanatenga asilimia moja ya faida yao kurejesha kwa jamii kupitia programu ya uwajibikaji na kwa miaka 10 wametoa zaidi ya Sh. bilioni 20 katika afya na elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi aliishukuru NMB kwa mkataba wa ushirikiano na uwekezaji iliyofanya katika jengo la uzazi la NMB