NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KLABU ya soka ya Azam Fc imetinga fainali za michuano ya Azam Sports Federation Cup baada ya kuilaza Simba kwa magoli 2-1.
Zikicheza kwa kuviziana huku kila mmoja akiwa na uchu wa kunyakua kombe baada ya kukata tamaa ya kunyakua kombe la ligi kuu, Azam ndio walikuwa wa kwanza kufumania nyavu za Simba baada ya Mwaikenda kukwamisha wavuni mpira dakika ya 22 ya mchezo.
Simba haikukubali kwani dakika sita baadaye, Kanoute aliisawazishia Simba goli na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare.
Dakika ya 75, ubao wa magoli ulibadilika ambapo mshambuliaji makini, Dube aliipatia Azam goli la pili ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
Azam inamsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili itakayoikutanisha Yanga na Singida Big Stars ili wanyukane kwenye fainali ya kombe hilo.