NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amehimiza viongozi wa dini watumie mafundisho yao kuzinusuru familia na wimbi la madai ya talaka.
Dk Mpango alisema hayo jijini Dodoma Jumapili wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Christian Ndosa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma.
Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk Fredrick Shoo.
Askofu Ndosa anachukua nafasi hiyo kwa kuwa Askofu Amon Kinyunyu ameistaafu baada ya kuiongoza dayosisi hiyo tangu mwaka 2012.
“Vilevile siku hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kesi ya madai ya talaka, ndo kuvunjika, wajane na yatima kunyang’anywa mali zilizoachwa na wenza au wazazi wao kinyume na mafundisho ya dini zetu,” alisema Dk Mpango na akaongeza:
”Kutokana na migogoro hiyo, familia nyingi zimeathirika na kuacha akina mama na watoto wakiteseka, mmomonyoko wa maadili tunaoushuhudia leo, kwa kiasi kikubwa unachangiwa na malezi mabaya, kuvunjika kwa taasisi ya ndoa na matumizi holela ya mitandao ya kijamii.”
Dk Mpango alisema dalili za mmomonyoko wa maadili zinaonekana hata kwa baadhi ya viongozi na waumini wa madhehebu ya dini wanaoenenda kinyume na mafundisho ya kweli ya dini.
Alisema kuna baadhi ya viongozi hao wa dini wanaharibu taswira nzuri ya jamii kupitia mafundisho na mienendo yao isiyofaa katika jamii.
Pia alisema bado kuna migogoro kwenye baadhi ya makanisa na misikiti, hivyo akatoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuhakikisha wanamaliza tofauti zao badala ya kufikisha mahakamani kwa kuwa hata mahakama ilishazisihi taasisi za dini kutopeleka migogoro yao mahakamani kabla ya kuzisuluhisha wao wenyewe.
Pia alisema kumekuwa na matumizi ya mabaya ya saluni ambapo baadhi ya watu huenda saluni usiku wa manane kufanyiwa masaji jambo ambalo si sawa.
Wakati akiwasilisha hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 bungeni hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, alisema Wizara hiyo kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) inaendelea na usajili wa matukio ya ndoa na talaka.
Dk Ndumbaro alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, RITA ilipokea marejesho 31,379 ya ndoa zilizofungwa na nakala za hukumu za talaka 410 na kusajiliwa.
Aidha, Askofu Shoo aliisihi serikali kuendelea kuwa wakali kwa watu wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu katika miradi ya kimkakati kwa kuwa fedha hizo ni kodi za wananchi.
“Shughulikieni kwa ukali, miradi hii ikiandamwa na ubadhirifu itanyong’onyeza wengi, lakini pia ni kukosa uzalendo na kuliumiza taifa, ni matumizi mabaya ya kodi za wananchi, zinapaswa zitumike na kusimamiwa vizuri badala ya kuwanufaisha wachache,”alisema Dk Shoo.
Askofu Ndosa aliipongeza serikali ya Rais Samia kwa kuendesha siasa za maridhiano na akaiomba kuwapatia eneo la wazi jirani na kanisa hilo mkoani Dodoma ili litumike kwa shughuli za kanisa na akaomba pia eneo la kujenga kitega uchumi Ihumwa.
Baada ya kuwekwa wakfu, Askofu Ndosa alimwingiza kazini, mchungaji Stanley Tabulu ili awe msaidizi wa askofu wa dayosisi hiyo.