NA JANETH JOVIN,ARUSHA
MITANDAO ya kijamii imekuwa ikitusaidia kupata habari na kuwaungaisha watu kutoka kila pembe za dunia na kuwapa jukwaa la kutuma ujumbe au kuwasiliana.
Kuandika habari ili kudanganya au kuburudisha watu kwa nyakati za sasa si kitu kipya, hata hivyo uwepo wa mitandaoni hii ya kijamii imesababisha habari feki na za kweli kuletwa kwa jamii kwa wakati mmoja na kwa njia ile ile ambapo wakati mwingine ni vigumu kutofautisha kweli na feki.
Habari hizi za uzushi au feki zimekuwa zinasambazwa haraka, hasa katika mtandao wa intaneti
Takwimu nchini Tanzania zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka 2022 zilionesha kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 watumiaji wa huduma za intaneti wameongezeka kwa asilimia 6.7 kutoka watu 29.1 milioni mwezi Juni hadi watu 31.1 Septemba.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ilieleza kuwa, ongezeko la watumiaji wa intaneti limeongezeka kwa matumizi ya intanenti kutoka wastani wa Megabaiti 6,037 kwa mtumiaji Machi mwaka huu hadi 6,626 kwa mtumiaji kwa mwezi Septemba.
Ni wazi kuwa ongezeko hilo linafana watu wengi kupata taarifa ambazo zingine ni feki na ili kuweza kukabiliana na tatizo hili ni muhimu kwa vyombo vya habari nchini viwe na uwezo wa kuchuja taarifa na waandishi kujitahidi kuzichambua kabla ya kuzisambaza.
Katika kuhakikisha waandishi wa habari wanapata elimu na kutambua mbinu za kuhakiki habari, picha na video zisizo za kweli, Shirika huru, lisilo la faida la Africa Check kwa kushirikiana na Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa waliamua kuandaa mafunzo kwa waandishi ya uhakiki wa habari.
Mafunzo hayo ya uhakiki wa habari Masterclass ambayo yalikuwa ya siku mbili yaliwakutanisha waandishi wa habari kutoka mkoa wa Shinyanga, Tabora, Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Geita na Iringa.
Alphonce Shiundu ni Mkufunzi kutoka Shirika huru, lisilo la faida la Africa Check akitoa mada katika mafunzo hayo anasema waandishi wa habari wanatakiwa kuhakiki kazi zao kabla ya kuzichapisha au kuziripoti katika mitandao ya kijamii au kwenye vyombo vyao vingine ili kuepukana na taarifa za uongo zenye lengo la kupotosha umma.
Shiundu anasema kumekuwa na uporoshaji mwingi wa habari katika mitadao ya kijamii na ili kuweza kuepukana na janga hilo muhimu waandishi wa habari kujifunza mbinu mbalimbali za kuweza kuzitambua ili wasije kuingia katika mtego wa kuzisambaza.
Anasema shirika lao limekuwa likizunguka maeneo mbalimbali katika nchi za Afrika kwa lengo la kuwaelimisha waandishi wa habari kutambua habari, picha na video zisizo za kweli.
“Africa Check tunatoa mafunzo haya ya uhakiki ya habari kwa waandishi wa Tanzania lengo ni kuwajenga wawe na uwezo wa kutambua habari, picha au video vya uongo ili kuziepuka, tunatambua mafunzo haya ni muhimu hivyo wote waliopata fursa ya kuyapata wahakikishe yanayatumia kwa vitendo kwa kuhakikisha habari watakazozitoa zinakuwa za kweli na uhakika,” anasema Shiundu
Anasema watu wanaofanya kazi za kusambaza habari za uongo wamekuwa wakibuni mbinu mpya kila siku hivyo ni muhimu kwa waandishi wa habari kusoma.na kujifunza kila siku namna ya kuweza kukabiliana na kundi hilo.
Naye Makinia Juma ambaye pia ni mkufunzi katika semina hiyo kutoka Africa Check, anasema ni muhimu waandishi wakatumia njia mbalimbali kuthibitisha habari au picha ambazo wanazilitilia mashaka kabla ya kuzisambaza au kuziripoti katika vyombo vyao vya habari.
“Kuna njia inajulikana na ‘Google image’, TinEye au RevEye hizo zote zinaweza kutumika kuthibitisha picha au habari ambayo mwandishi atakuwa hana uhakika nayo, waandishi waliopata fursa kuja katika mafunzo haya tumewafundisha kwa kina namna ya kuzitumia njia hizi, kilichobaki ni kufanya mazoezi mara kwa mara,” anasema Juma
Anasema Africa Check itaendelea kutoa mafunzo wa Wanahabari kadiri watakavyokuwa wakipata nafasi ya kufanya hivyo lengo kuondokana na usambazaji wa habari feki katika vyombo vya habari.
“Tunataka ifike mahali kila mwandishi wa habari kabla ya kusambaza habari anayoiona katika mtandao anaihakiki kwanza kwa kutumia njia ambazo atakuwa amefundishwa,” anasema
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha mafunzo wa Nukta Africa, Daniel Mwingira anasema mafunzo ya uhakiki wa habari ni muhimu kwa wanahabari nchini Tanzania kwa sababu wanapata mbinu mbalimbali hasa za kidijitali kuwawezesha kuhakiki na kuzalisha habari zenye ubora wa hali ya juu.
“Dunia inaenda kwa kasi na Tanzania siyo kisiwa hivyo wanahabari wanapaswa kupata maarifa mapya ili waweze kuboresha habari zao na kuandika habari zenye manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla,” anasema Mwingira.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Asha Mwakyonde na Shabani Njia walikiri kwamba yatawasaidia kuboresha uandishi wao wa habari hususani kutumia njia walizofundishwa kuhakiki habari kabla ya kuchapishwa mtandaoni.
Hata hivyo Mwakyonde anasema kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa wanahabari kunachangia kuwepo kwa usambazaji wa habari hizo zisizo za kweli.
Anasema licha ya wasambazaji hao wa habari feki kubuni mbinu mpya kila kukicha lakini jamii inapaswa kupewa elimu ya kuweza kukabiliana nao na hatua za kuchukua pindi wanapokutana na habari au picha mitandaoni.