NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JUMLA ya watahiniwa 106,955 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita utakaofanyika kuanzia Mei 2 hadi 22 mwaka huu.
Mtihani huo utaenda sambamba na mtihani wa ualimu utakaofanyika kati ya Mei 2 hadi 16 mwaka huu ambapo jumla ya watahiniwa 8,906 wamesajiliwa.
Akitangaza kuhusu kuanza kwa mitihani hiyo leo Aprili 30, 2023 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Dk Said Mohamed amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani husika katika vituo.
Dk Mohamed ametumia nafasi hiyo kuzitaka kamati za mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha taratibu za uendeshaji mitihani ya Taifa inazingatiwa.
“Kamati zihakikishe mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu. Wasimamizi nao watekeleze majukumu yao kwa weledi na kuzingatia kanuni za mitihani.
“Kwa upande wa watahiniwa, Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vyema hivyo ni matarajio yetu watafanya mitihani kwa kuzingatia kanuni za mitihani huku wakijiepusha na vitendo vya udanganyifu,” amesema Dk Mohamed.