NA MWANDISHI WETU, MWANZA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, ameambatana na wataalam mbalimbali wakiwemo wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Afisa Ustawi Wilaya ya Magu, kuchunguza tukio la mtoto, Mabilika Wilson, mwenye umri wa miaka minane anayedaiwa kufa, kuzikwa, kisha kuonekana akiwa hai.
Kwa mujibu wa kamanda, kifo cha mtoto huo kilitokea April 16 mwaka huu katika kijiji cha Salong’we, Kata ya Mwamabanza, Wilaya ya Magu na maziko kufanyika kesho yake.
Aprili 27 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni, marehemu akaripotiwa kuonekana kijijini Mwangika, Kata ya Mwabomba, Wilaya ya Kwimba baada ya vijana waliokuwa wakichunga ng’ombe kumuona moto huyo akiwa anahangaika porini peke yake.
Mtoto aliweza kutoa ushirikiano kwa kujieleza vizuri kwao ni wapi, polisi ikazifanyia kazi taarifa hizo kwa kuwatafuta wazazi wake, Wilson Bulabo na Helena Robert, wilayani Magu.
“Wazazi wote walimtambua Mabilika kuwa ni mtoto wao na kukiri kwamba alifariki na kuzikwa. Kwa mkanganyiko huo, Polisi na timu nzima tukachukua hatua ya kufukua kaburi,” amesema Mutafungwa na kuongeza:
Kaburini kulikua na mwili ambao wazazi walisema sio wa mtoto wao, isipokuwa aliyeokotwa wilayani Kwimba ndiye mtoto wao halisi.
Mwili uliokutwa kaburini umechukuliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi, ikiwemo kutambua uhusiano wa maiti iliyokutwa kaburini na mtoto aliyeokotwa wilayani Magu.