NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema kuwa zaidi ya wageni 20,000 wanatarajiwa kuingia nchini kushuhudia mashindano ya 74 ya Miss World 2027 yatakayofanyika nchini mwakani.
Makonda ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 20,2026 wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya kimataifa ya urembo.
Amesema kuwa wakati wa fainali za mashindano hayo, vyombo mbalimbali vya habari duniani vitarusha matangazo yatakayofuatiliwa na takribani watazamaji Bilioni mbili, hali itakayotoa fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa.
Ameeleza kuwa hatua ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Miss World ni ya kihistoria, kwani inaifanya kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika kuandaa mashindano hayo makubwa ya urembo duniani.
Makonda amesema kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa muda wa siku 28, ambapo yatahusisha matukio mbalimbali ikiwemo sherehe ya ufunguzi, chakula cha wageni, mashindano ya vipaji, chakula cha hisani, maonesho ya mitindo pamoja na fainali ya mashindano hayo.
Kutokana na ukubwa wa tukio hilo, Waziri Makonda amewataka wafanyabiashara nchini kujipanga mapema ili kutumia fursa ya kiuchumi itakayotokana na uwepo wa wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha, amewataka warembo wanaoshiriki mashindano mbalimbali nchini kuzingatia maadili na kutunza heshima wanayopewa, ili kujenga imani kwa jamii ikiwemo wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika mashindano hayo.
Pia ametoa wito kwa wadau na wafadhili kuunga mkono waandaaji wa mashindano ya urembo nchini ili kuyawezesha kufanyika kwa viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ujio wa mashindano hayo ni fursa kubwa kwa Tanzania kuendelea kujitangaza kimataifa kupitia sekta ya utalii, utamaduni na sanaa.



