NA MWANDISHI WETU, LINDI
JESHI la Polisi wilaya ya Nachingwea limesema limepokea taarifa za raia wa kigeni mwenye asili ya India kuwatishia watu bastola mgodini hivyo uchunguzi unaendelea kufanyika kwani ni kinyume na sheria za nchi.
Aidha limesema kuwa hakuna mwananchi yeyote yule mwenyewe ruhusa ya kuwatishia bastola au kupiga risasi hadhara bila kuwa ruhusa au unakumbana na madhara hivyo wananchi wanatakiwa kutoa taarifa mapema waposikia tena milio ya risasi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohamed Moyo kwenye mgodi wa Nditi,Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nachingwea James Chacha amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda na amani na utulivu uliopo kwenye mgodi huo.
Chacha aliwataka wachimbaji wa madini katika mgodi wa Nditi kuhakikisha wanalinda amani na utulivu ili shughuli za uchimbaji wa madini uendelee kwa amani.
Aidha Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nachingwea Chacha alimalizia kwa kuwataka wachimbaji wadogo wadogo kuacha kuiba madini ya wachimbaji wakubwa kwa kufanya hivyo kunawapelekea hasara wachimbaji hao
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nachingwea Moyo aliagiza kujengwa kwa kituo cha Polisi katika machimbo ya madini ya Nditi ndani ya siku 14 ili kuondoa migogoro inayoendelea katika mgodi huo.