NA MWANDISHI WETU
KAMANDA wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Mary Kipesha amesema wamekamata watuhumiwa sita wakiwa na kilo 17.14 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Kamanda huyo aliyasema hayo Aprili 28, 2023 alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya viwanja vya ndege Dar es Salaam.
Akitolea ufafanuzi namna watuhumiwa hao walivyodakwa akiwemo mzee wa miaka 74 aliyefunga bangi kwenye kiuno, alisema ni kutokana na vifaa vya kisasa walivyonavyo ambavyo hufanya kazi kwa ufanisi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni abiria mmoja wa kiume (43) ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, ambaye Machi 29, 2023 saa 1:40 usiku alikamatwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jengo la tatu la abiria eneo la ukaguzi wa mwisho akiwa na kilo 2.25 za bangi akijiandaa kusafiri kwenda Dubai kwa Shirika la Ndege la Fly Dubai.
Kadhalika Aprili 14, 2023 majira ya 12:30 jioni huko katika Jengo la tatu la abiria la uwanja huo, abiria aliyekuwa anatarajia kusafiri kwenda Dubai kupitia Zanzibar kwa ndege ya Fly Dubai alidakwa akiwa na pakiti nne za bangi zenye kilo 3.16.
Wengine ni mwanaume mmoja wa miaka 34 aliyedakwa Aprili 14, 2023 saa 7:15 mchana akiwa na kilo 2.8 za bangi akitarajia kusafiri kwenda Dubai kwa ndege ya Emirates.
Aprili 16, mwaka huu saa 1:30 usiku mwanaume mmoja miaka 58 alidakwa akiwa na kilo 3.764 za bangi akielekea Dubai kwa ndege ya Fly Dubai.
Vilevile Aprili 17, mwaka huu saa 12:30 jioni, Rehema Ally (42) alikamatwa na kilo 1.5 naye akijiandaa kuelekea Dubai kupitia Zanzibar.
Pia alikuwepo Mohamed Kumkana (74) aliyekamatwa Aprili 17, mwaka huu akiwa na kilo 3.66 akielekea Dubai na Fly Dubai.