NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya viwandani na wadau wa sekta hiyo zaidi ya 700 wanatarajiwa kukutana leo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili ikiwemo ya viwanda vilivyopo nchini kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi na si kuchukua zile zilizopo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Aprili 4, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Dk. Venance Mwasse wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano huo unaotarajiwa kufanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Mwasse amesema wanataka kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa viwanda lakini ili kuweza kuifikia azma hiyo ni muhimu kutatua changamoto hiyo ya wamiliki wa viwanda nchini kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga amesema wanafahamu kuwa wenye viwanda wanahitaji ubora hivyo kupitia mkutano huo wataeleza na kuhojiwa ni kwanini viwanda vyao havitumii malighafi za hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania (TAWOWA) Salma Ernest amesema wanawake wanauona mkutano huo ni fursa kwao kwani utakwenda kutatua masuala yaliyokuwa yakiwakwamisha kupiga hatua katika biashara hiyo.