KINSHASA, DR CONGO
JANETH Magufuli, mjane wa aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, hayati John Pombe Magufuli ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya Kimataifa toleo la tatu, inayotolewa na taasisi ya Martha Tshisekedi Kasalu (M. T. Kasalu).
Mama Janeth amepata tuzo hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake kwa Taifa la Tanzania na kwa hayati Rais Magufuli akiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati akitekeleza majukumu yake Kitaifa na Kimataifa.
Tuzo hiyo ni maalum kwa wenza wa viongozi wakuu wa nchi na watu maarufu duniani kwa kutambua michango yao kwa wenza wao, jamii na taifa husika.
Tuzo hiyo ambayo hufahamika rasmi kama M. T. Kasalu, Femme D’Honneur Trophee, ilitolewa jana Ijumaa Machi 24, 2023 katika hoteli ya Pullman jijini Kinshasa.
Waandaaji wa Tuzo hii ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Urithi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakishirikiana na Taasisi ya Lizadeel.

Kwa mwaka huu 2023 waliopokea tuzo hii ni;
1. Mama Janeth Magufuli (Tanzania) – Mchango wake kwa Rais wa Awamu ya Tano unafahamika Afrika na duniani kote.
2. Mama Suzanne Mukay (Congo) – Mke wa Daktari maarufu nchini DRC, wa magonjwa ya kina wanawake na kansa, ambapo mumewe ameisaidia jamii kwenye nyanja hizo.
3. Mama Vivianne Dalo (DRC) – Mke wa Mchungaji Maarufu na anayeheshimika nchini DRC, Pastor Roland Dalo. Amesaidia jamii hasa wajane, yatima na vijana katika kujitegemea.
4. Mama Colette Senghor (Senegal) – Mke wa Rais wa kwanza wa Senegal, Leopold Sedar Senghor , aliisaidia Senegal kupata Uhuru.
5. Mama Coretta King (USA) – Mke wa Martin Luther King. Mumewe alisaidia mengi ikiwemo kupinga ubaguzi wa rangi Marekani