NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAKALA wa Vipimo (WMA) wameanza kutoa elimu ya vipimo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi katika siku ya kwanza, (Agosti 1, 2026) ya Maonesho ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya John Malecela, eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
Kwenye banda lake lenye kaulimbiu
“Usahihi wa Vipimo vya Mbegu, Pembejeo, Mazao na Bidhaa Sokoni ni Msingi wa Tija na Utekelezaji wa Dira 2050,” Maafisa Vipimo wa WMA wanatoa elimu ya vipimo na majukumu ya Wakala kwa ujumla katika kulinda haki za wakulima, wafugaji, wavuvi na wanunuzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA Veronica Simba alisema lengo ni kuhakikisha kila mkulima, mfugaji na mvuvi anaelewa umuhimu wa kutumia mizani na vipimo vingine vilivyohakikiwa na WMA.
“Kama unauza mahindi, mbolea au maziwa, na kama unanunua pembejeo za mifugo au samaki, kipimo sahihi ndiyo msingi wa faida. Tunataka kila mtu atoke hapa Nane Nane akiwa na uelewa wa kutambua na kudai kipimo sahihi,” alisisitiza Simba
Simba aliwataka wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla kutembelea banda la WMA katika kipindi chote cha maonesho hayo. “Wataalamu wetu wapo hapa kutoa elimu bure. Njoo ujifunze, uulize maswali na hata kutoa maoni yako,” aliongeza.
WMA imesema itatumia kipindi chote cha maonesho hayo kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi kama njia moja ya kutekeleza Kauli Mbiu ya Taifa ya NaneNane 2026 “Tambua Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050” na kuhakikisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi inakuwa na ushindani na uhakika wa soko.





