PRETORIA, AFRIKA KUSINI
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, jana Jumatatu, Machi 20, 2023 alifanikiwa kuwaingiza watu barararani kwenye maandamano ya Amani yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Wiki iliyopita, EFF ambacho ni chama cha tatu kwa ukubwa nchini Afrika Kusini kilitoa taarifa kwa umma ikiutaka usiende makazini badala yake waende barabarani kuandamana.
Makampuni mbalimbali nayo yalitoa taarifa kwa wafanyakazi wao wakiwataarifu kusalia nyumbani siku hiyo.
Polisi walitawanywa jana kwenye maeneo mbalimbali nchini humo baada ya chama hicho cha mrengo wa kushoto kutoa wito wa maandamano ya kitaifa. Kumekuwa na hofu ya kushuhudiwa kwa mara nyingine machafuko ambayo yalisababisha vifo miaka miwili iliyopita.
Bunge la nchini humo lilitangaza kuwa Rais Cyril Ramaphosa ameidhinisha wanajeshi 3,474 kuungana na polisi katika kudhibiti maandamano hayo.
Takribani waandamanaji 87 walikamatwa jana kwenye maandamano hayo ambayo chanzo chake ni mgao wa umeme na kupanda kwa gharama za maisha.
Wito huo wa maandamano umeibua kumbukumbu za ghasia za Julai, 2021, kulipotokea ghasia mbaya zaidi kushuhudiwa tangu mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, ambapo watu wasiopungua 350 waliuawa katika maandamano yaliyochochewa na kitendo cha kufungwa kwa rais wa zamani Jacob Zuma na kusababisha ghasia na uporaji. Ramaphosa ameagiza vyombo vya sheria kuhakikisha hakuna marudio ya machafuko ya mwaka 2021.