NA EDNA BONDO, ARUSHA
SIKU kadhaa zilizopita Shirika la Bima la Taifa (NIC) lilizindua Bima mpya iitwayo Beam Life.
Ili kufahamu kwa undani kuhusu bima hii mpya Demokrasia lilifanya mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Bima ya Maisha wa NIC Hardbert Polepole.
Na Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo;
Swali:BeamLife ni nini?
Jibu:Ni Bima ya Maisha inayotoa riba shindani kwa fedha zilizowekwa kidogo kidogoau kwa mkupuo.Ni aina ya Bima ambayo mteja huweza kunufaika iwapo itatokea mke, mume , watoto au yeye mwenyewe akifikwa na umauti.
Swali:Nini faida ya BeamLife?
Jibu:Faida yake ni kuongeza ukwasi na fidia kutokana na msiba
Swali:Ni makundi gani yanaweza kujiunga na BeamLife?
Jibu:Makundi yote au watu wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi wanaweza kujiunga na bima hii.Hii ina maana ya kwamba raia yeyote wa Tanzania anayeishi ndani au nje ya nchi anaweza kujiunga cha msingi awe na miaka 18 hadi 75.
Swali:Kiwango cha kuchangia BeamLife ni kiasi gani?
Jibu:Kiwango cha chini sh.5, 000 hadi sh.2, 000, 000 kwa michango ya mkupuo.Na katika hii michango mtu anaweza kuchangia kati ya miaka mitano hadi 15.Lakini pia mtu anaweza kuchagua namna ya kuchangia ikiwamo mwezi, miezi mitatu, miezi sita au mwaka kulingana na uwezo wake.
Swali:Mteja huchangia kwa njia gani?
Jibu:Mwanachama anaweza kuchangia kupitia kwa mwajiri, benki, mitandao ya simu nk
Swali:Ni kwa namna gani mteja anaweza kupata taarifa za michango yake?
Jibu:Taarifa hupatikana kwa njia ya intaneti, simu au kufika katika ofisi za NIC zilizopo Tanzania nzima.
Swali:Je mteja akishindwa kuchangia afanye nini?
Jibu:Hutakiwa kuacha kuchangia na kusubiri hadi mwisho wa mkataba au anaweza kupunguza michango na kuendelea kiasi anachoweza kunudu lakini pia anaweza kujitoa kwa kuomba salio lililopo.
Kujitoa kunaweza kufanyika baada ya mteja kutimiza miaka mitatu.
Swali:Mteja akisitisha kuchangia anaweza kupata faida?
Jibu:Ndio, atapata faida ya uwekezaji tu
Swali;Mteja atajuaje kama bima yake imeiva?
Jibu:Taarifa za kuiva kwa Bima zimeandikwa kwenye mkataba wa mteja na shirika hivyo shirika litawajibika kutoa taarifa kwa mteja ili taratibu za malipo zifanyike kwa wakati amnapo malipo yatalipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mteja.
Swali:Nini Matarajio ya uwekezaji katika BeamLife?
Jibu:Matarajio ni jumla ya michango na riba inayopaswa kulipwa na mteja baada ya kumaliza muda wa kuchangia.
Swali:Ni wakati gani na ni nani atalipwa fidia ya rambirambi?
Jibu:Endapo mteja atafariki rambirambi itatolewa kwa wategemezi wake.Endapo mtegemezi(mke, watoto)atafariki mteja ndiye atakayelipwa rambirambi kulingana na muingozo wa sheria.
Swali:Iwapo mteja atafariki , Je bima itaendelea?
Jibu:Hapana, Bima itakoma mara tu mteja atakapofariki hivyo wategemezi wake ambao ni mke na watoto watalipwa fidia ya rambirambi, michango na faida itokanayo na uwekezaji kwa wakati mmoja ambayo itakuwa ni asilimia tano ya matarajio ya uwekezaji wa mteja.
Lakini pia ikumbukwe kwamba fidia hutolewa mara moja tu kwa mwaka.
Swali:Ni nyaraka gani hutakiwa katika madai ya fidia au mafao ya BeamLife?
Jibu:Nyaraka zinazotakiwa ni kibali cha mazishi, cheti cha kifo na nakala ya hati ya bima na kwa upande wa mafao ya BeamLife ni hati ya bima tu ndio huhitajika.
Swali:Je mteja akipata fidia ya rambirambi, mafao yake ya uwekezaji yanaathirika?
Jibu:Hapana, hakuna uhusiano wa mafao ya uwekezaji na fidia ya rambi rambi.
Hata mteja alilipwa rambirambi bado michango na mafao yatokanayo na uwekezaji yataendelea kuwepo.
Swali:Hadi sasa BeamLife ina wateja wangapi sokoni?
Jibu:Tayari BeamLife ambayo tumeipa kauli mbiu ya mshkaji wa kweli ina wateja zaidi ya 2000 …na hii ni kabla hata haijazinduliwa .
“Hii ni ishara njema ya uwepo wa BeamLife sokoni hivyo matarajio ya ongezeko la idadi ya wateja kwa mwaka ujao ni kubwa mno kwasababu NIC ni shirika linalotoa huduma zenye viwango kutokana na ukwasi ilionao”
Caption
Mkurugenzi wa Bima za Maisha (NIC) Hardbet Polepole akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya BeamLife