NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Klabu ya Simba umethibisha kuwa katika mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar itakosa huduma ya wachezaji wake watu ambao wanakabiliwa na changamoto ya kuwa majeruhi baada ya kuumia katika moja ya michezo ambayo wamecheza.
Meneja wa Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amewataja wachezaji hao kuwa ni Kibu Denis aliyepata majeraha katika mchezo dhidi ya Vipers uliochezwa wiki mbili zilizopita nchini Uganda na Simba kuibuika na ushindi wa bao 1-0.
Wachezaji wengine watakaokosekana ni Augustine Okrah na Isamel Sawadogo ingawa hali zao zinaendelea vizuri na pindi watakapokuwa sawasawa zaidi watarejea kwenye kikosi hicho ili kupambania timu na kuifikisha katika malengo yake kwenye michezo ya ndani na kimataifa.
Simba inashuka katika dimba la Manungu mkoani Morogoro Machi 11, 2023 dhidi ya Mtibwa kusaka alama ili kuifukuza Yanga inayopunga upepo na alama zake 62 huku ‘Mnyama’ akiwa na alama 54 na tofauti yao ikiwa ni alama nane.