NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA
MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Old Shinyanga Rashid Mashaka (14 )amepoteza maisha baada ya nyumba aliyokuwa amelala kuungua moto.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 10 majira ya saa 6 usiku katika kitongoji cha Senyenge kata ya Old Shinyanga baada ya hitilafu ya umeme kutokea katika nyumba hiyo kisha moto kuwaka na kuunguza vitu mbalimbali wakati kijana huyo akiwa amelala ndani.
Mama mzazi wa marehemu huyo, Fatuma Rajab ambaye hakuwepo nyumbani wakati wa tukio hilo amesema mvua zilizonyesha jana zilisababisha umeme kukatika na uliporejea majira hayo ndipo hitilafu hiyo ilitokea kisha nyumba yake kushika moto.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Shinyanga Inspekta Stanley Luhwago amesema kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye mita ya nyumba hiyo.